Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA),
wamepongeza ufanisi wa kazi unaofanywa kwa pamoja baina ya Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA), huku wakizitaka nchi wanachama wa
Jumuiya hiyo, kuhakikisha wanaunganisha reli za nchi zao ili kuongeza kasi ya
uchukuzi na usafirishaji wa mizigo.
Hayo
yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Spika wa Bunge hilo kwa niaba ya
wabunge hao, Dk Margaret Zziwa wakati walipofanya ziara kwenye bandari ya Dar
es Salaam, kuona jinsi kazi zinavyoendeshwa.
Zziwa alisema ni
wazi kwamba TPA na TRA wanafanya kazi nzuri inayohitaji pongezi na kwamba kwa
ufanisi huo wameona mafanikio ya kuwa na jumuiya hiyo.
Alishauri nchi
za jumuiya hiyo ambazo hazina reli zinazofanya kazi kuhakikisha zinafufuliwa au
kujengwa na kuhakikisha zinajengwa na kuunganisha na reli za nchi nyingine ili
kufanikisha huduma za uchukuzi na usafirishaji wa mizigo kutoka na kwenda
bandarini.
Kwa upande wake,
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bandari wa TPA, Awadh Massawe alisema ufanisi wa kazi
bandarini umeongezeka na kwamba hivi sasa uondoshaji mizigo katika bandari hiyo
hutumia kati ya siku mbili hadi tano, na kwamba hiyo inasaidia kupunguza
gharama zisizo za msingi wa wafanyabiashara na ndani na wa nchi jirani.
Hata hivyo,
alisema pamoja na ufanisi wa sasa bado Mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto
nyingi ikiwamo ya usafirishaji wa mizigo, ambapo kwa hivi sasa asilimia 99 ya
mizigo yote bandarini inabebwa kwa njia ya magari.
Akizungumzia
mfumo mpya wa Himaya Moja ya Forodha (SCT) kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Kamishna Mkuu wa TRA, Lusekelo Mwaseba alisema mfumo huo ulioanza kufanya kazi
mwezi Julai mwaka huu, utapunguza gharama za wafanyabiashara na pia utaondoa
ufanyaji mara mbili wa taratibu za uondoshaji mizigo.
No comments:
Post a Comment