Shahidi wa kwanza katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayowakabili wafanyabiashara watatu, ameieleza mahakama jinsi alivyotapeliwa na wafanyabiashara hao.
Mfanyabiashara wa vyombo na nguo, Tamal Daniel (44) alitoa ushahidi huo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mbele ya Hakimu, Wilberforce Luhwago.
Daniel aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Joyce Winla (32), Emmanuel Mwakasala (36) na Evetha Herman (32), wote wafanyabiashara.
Alidai kwamba yeye ni mfanyabiashara anayetoa bidhaa Dar es Salaam na kuzisafirisha jijini Mbeya na kwamba aliyekuwa akimsafirishia mizigo hiyo ni mfanyabiashara mwenzake Mwakasala.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, Daniel alidai Oktoba 22 mwaka 2011, wakati yupo jijini hapa, Mwakasala alimtambulisha kwa mfanyabiashara mwenzao anayeitwa Winla ambaye ni mtuhumiwa namba moja katika kesi hiyo ni msafirishaji wa vyombo kwenda nchini Angola.
Alidai baada ya utambulisho huo, alipigiwa simu na Winla na kumtaarifu kwamba ana shida na Sh milioni saba kwa kuwa mzigo wake umekwama bandarini na kwamba hana fedha kwa ajili ya kutolea mzigo huo.
Shahidi huyo alidai Mwakasala alimhakikishia kwamba Winla ni mfanyabiashara ambaye walijuana na ni mwaminifu kwamba ana magari aina ya Noah na Toyota Double Coaster, mashamba na duka la nguo lililopo maeneo ya Kariakoo.
Aliendelea kudai walikubaliana kwamba atakapotoa fedha hizo, mzigo utakapotoka bandarini atapatiwa na pia alipewa gari aina ya Noah kama dhamana ya fedha atakazochukua Winla.
Daniel alidai Winla alimuonesha duka lake la nguo lililopo Kariakoo na walimkuta mtuhumiwa namba tatu ambaye ni Herman na kumtambulisha kuwa ndiye anayemuuzia na kufuata mizigo Nairobi, Kenya.
Pia alidai waliongozana na Winla hadi Benki ya NMB tawi la Kariakoo na kutoa Sh milioni saba ndipo Winla alimuita wakala wake na kushuhudia makabidhiano hayo na baadaye alimpigia simu Mwakasala kumtaarifu kuwa amempatia Winla fedha hizo.
Baada ya makubaliano hayo, Daniel alirudi Mbeya na kwamba aliahidiwa baada ya siku nne mzigo utakuwa tayari. Alidai alisubiri hadi siku hizo zilipofika na kumpigia simu Mwakasala kumuuliza kama mzigo tayari, lakini aliambiwa kwamba mzigo huo bado huku Winla akiwa hapatikani katika simu yake.
Hata hivyo, alidai baada ya wiki hakukuta gari aliloliacha kwa Mwakasala na kudai kuwa gari hilo alikuwa amelichukua Winla kwenda nalo Kibaha katika mashamba yake.
Alidai baada ya kutopatikana kwa washitakiwa hao, aliripoti katika kituo cha Polisi cha Msimbazi na kufanikiwa kuwakamata. Walipokamatwa wakala wa mshitakiwa wa kwanza alidai mbele ya Polisi kwamba fedha hizo walizitumia kwa mahitaji yao.
Washitakiwa hao walidaiwa Oktoba 25 mwaka 2011, maeneo ya mtaa wa Livingstone, Kariakoo, Dar es Salaam, walikula njama kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Pia walidaiwa walijipatia Sh milioni 7 kutoka kwa Tamal Daniel, kwa kumdanganya kwamba watamrudishia baada ya siku nne huku wakijua sio kweli. Washitakiwa walikana na wapo nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment