Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege, amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kutoa msamaha wa ada ya utawala kwa kampuni mbili bila kibali.
Aidha Mahakama imeamuru Ekelege kurudisha Sh milioni 68 alizolisababishia hasara shirika hilo, kutokana na kutoa msamaha huo.
Ekelege alikuwa akikabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababishia shirika hilo hasara ya mamilioni hayo ya Shilingi, baada ya kuondoa ada ya asilimia 50, kwa Kampuni za Jaffar Mohamed Ali na Quality Motors bila idhini ya Bodi.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Augustina Mmbando, alitoa hukumu hiyo jana baada ya kuridhika na ushahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa naTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mmbando alisema mshitakiwa amepatikana na hatia katika mashitaka matatu na katika kila kosa, atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, sawa na miaka mitatu.\
Hata hivyo Ekelege atatumikia kifungo hicho kwa wakati mmoja, hivyo ni sawa na kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.\
Awali Wakili wa Takukuru, Janeth Machulya, aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwake na kwa viongozi wengine wanaotumia madaraka yao vibaya.
Lakini Wakili wa Ekelege, Majura Magafu, aliiomba Mahakama impunguzie mshitakiwa adhabu kwa kuwa anafamilia inayomtegemea.
Katika mashitaka yake, ilidaiwa kuwa kati ya Machi 28, mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, Ekelege alitumia madaraka vibaya kusamehe ada kampuni mbili kwa asilimia 50, ambayo ni sawa na Sh milioni 68 bila idhini ya Baraza la Utendaji, kinyume na utaratibu wa TBS.
Katika shitaka la pili na la tatu, alidaiwa kutoa msamaha kwa kampuni hizo na kusababishia shirika hilo hasara ya Sh milioni 68.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Ekelege alitoa msamaha huo bila kumshirikisha Meneja wa Fedha wala kupata kibali kutoka katika baraza hilo, ambalo kwa sasa limebadilishwa jina na kuwa Bodi ya Wakurugenzi.
No comments:
Post a Comment