SITTA AWAJIBU WANAOFANANISHA TUME YA WARIOBA NA BUNGE
Baada ya watu na
taasisi kadhaa kudai kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba kupokea maoni ya
wananchi na kuyaongeza kwenye rasimu ya Katiba mpya, ni kuingilia kazi ya Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta, alisema bunge
hilo lina mamlaka makubwa kuliko tume hiyo.
Amesema
hata wajumbe wa bunge hilo wanaoendelea kupitia rasimu hiyo, siyo mazuzu, wana
akili zao, wasomi na wapo watu wengi wanaotambua kazi hiyo na kuipongeza.
Sitta
alivunja ukimya huo na kutoa ufafanuzi jana mbele ya
waandishi
wa habari kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa, na kuongeza kuwa wananchi
wameona rasimu ya Katiba mpya, ina upungufu.
“Mimi
naelewa kuna watu wanakasirishwa sana na kazi tunayoendelea kuifanya, ni haki
yao kukasirika lakini kinachofanywa ni wananchi ambao hatukuwaalika, wanakuja
kwa makundi kuelezea wanachoona kuwa ni upungufu ndani ya rasimu, sasa haya
watayapeleka wapi?
“Hii
hali ya kuonekana sisi Bunge na Tume tupo hadhi moja si kweli, Tume ina mamlaka
yake lakini Bunge lina mamlaka makubwa zaidi ya Tume… waliotunga sheria waliona
ipo kazi inayofanyika pamoja na kufanya marekebisho ndio maana wanachotoa wao
ni rasimu sisi tutakachotoa inaitwa Katiba inayopendekezwa.”
Alisema
dhana kwamba lolote likifanywa kwenye rasimu ni usaliti kwa nchi au
inachakachuliwa, msingi wake ni ghadhabu za mtu na uamuzi tu wa kuwaona waliopo
Dodoma ni mazuzu.
“Hapa kuna watu wasomi
wazuri tu wenye akili zao. Kusema tunafanya kazi ya Tume ni upotoshaji mwingine
wa watu wasiotakia mema Bunge Maalumu la Katiba. Sijui kwa nini rasimu inapewa
hadhi kama msahafu, wakati imeandikwa na binadamu tu ina upungufu mkubwa. “Mtaona kuanzia Septemba 2 mijadala ya hoja itakavyokuwa.
Wananchi wao wameona Tume haikuwatendea haki maoni yao waliyoyatoa, na waliona mahali pa kwenda kwenye chombo cha juu zaidi nacho ni Bunge Maalumu la Katiba, tuna wajibu wa kuwapokea kwani tupo kwenye kazi ya kutunga Katiba”.
Alisema kazi inayofanyika, ni kutoa Katiba rafiki kwa wananchi na kutoa mfano wa wasanii, ambao waliona pamoja na kutoa maoni kwa maandishi, hayakuzingatiwa na Tume lakini Bunge kwa vigezo vyake, limeona inastahili.
“Wamekuja wakitaka kwenye rasimu kuwekwe kipengele cha mali isiyoshikika, yaani haki miliki bunifu nasi tumeona inastahili, lakini Tume waliiacha nasi tumeongezea kwenye sehemu rasimu iliyoweka mali tu,” alisema.
Miongoni mwa vipengele vilivyoongezwa kwenye rasimu hiyo, ni masuala ya Serikali za Mitaa, yaliyotokana na andiko la aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambayo yalipangwa kuwepo kwenye Katiba ya Serikali ya Tanganyika, ambayo ni ardhi, mazingira, rasilimali za Taifa na haki za watumiaji wa bidhaa.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu, alisema Kamati yake imeshapitisha sura zote kwa kupata theluthi mbili kila upande, lakini suala la akaunti ya pamoja kwa Tanzania Bara na Zanzibar, hawakufanya uamuzi.
Alisema wajumbe wa kamati hiyo, walitaka suala hilo liwekwe kiporo hadi baada ya kukamilika kwa semina ya wataalamu wa masuala ya fedha, waliokuwa wakiwapa jana kuhusu mgawanyo huo wa fedha.
“Tunataka tujue kwa sasa hali ikoje, changamoto zake na wapi kwenye kero. Kwenye suala hili wajumbe walibishana sana na waliweka pembeni itikadi za vyama vyao vya siasa,” alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba 11, Hamad Masauni Yusuf, alisema Kamati yake imeshapiga kura kwenye sura zote na changamoto kubwa waliyokumbana nayo, ni suala la fedha za pamoja.
“Leo (jana) tunategemea kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa fedha na tukiona kuna mambo muhimu, itatubidi tuitishe kikao cha dharura kufanya marekebisho. Lengo ni pamoja na masuala ya fedha. Pia Muungano uimarishwe na kusiwe na mambo ya kuutatiza na pande zote mbili zifaidike,” alisema.
Mwenyekiti Kamati Namba Nne, Christopher ole Sendeka, ambaye hakuwepo kwa muda mrefu kuhudhuria kamati kutokana na kuuguliwa na watu wa familia yake, alisema kutokuwepo kwake hakupaswi kuonekana kuwa anaunga mkono Ukawa.
Alisema kwenye kamati yake kulikuwa na mjadala mkali na watu walikuwa wakali lakini mwishowe walielewana vizuri.
Alitaja maeneo yaliyosababisha wajumbe kuwa wakali kuwa ni ardhi, uraia pacha, masuala ya wakulima na wafugaji na muundo wa Bunge.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis Michael, alisema kwenye Kamati yake walipingana sana na kuvutana na kufanikiwa kupata makubaliano mazuri na kila sura kupata theluthi mbili kwenye sura zote.
Comments