VIJANA 1,200 WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UCHIMBAJI MADINI


Vijana 1,200 watafaidika kupata mafunzo ya uchimbaji wa madini na gesi yatakayotolewa nchini kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Mambo ya Nje, Biashara na Maendeleo ya Canada (DIFATD).
Mafunzo hayo yatatolewa kwa miaka mitano kama mpango wa kuongeza fursa kwa wahitimu  kujiajiri, kushiriki katika Sekta ya Utalii na Uchimbaji wa Madini.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi, Thomas Katebalirwe.
Alisema mafunzo hayo yatatekeleza Mpango wa Mafunzo ya Kukuza Stadi kwa ajili ya Uajiri (ISTEP) ulioanzishwa na Asasi ya vyuo na taasisi za Canada.
Alisema taasisi 11 zitashirikiana kukuza uelewa kwa vijana kwani gesi ni kitu kipya kinachohitaji nguvu kazi ya kutosha na yenye mafunzo maalumu.
 ‘’Vijana hao watatoka katika taasisi za utalii na madini na gesi kuwapatia mafunzo ya uchimbaji wa madini na uchomeleaji wa mabomba ya gesi,’’ alisema Katebalirwe.
Naye Mwenyekiti kutoka Shirikisho la Wachimbaji na Watafutaji wa Madini Tanzania, Nyanda Shuli alisema mpango huo ni muhimu katika kuendeleza Sekta ya Madini  na Nishati kwa kuwa inahitaji nguvu kazi ya kutosha kukuza sekta hiyo.
Alisema kila mwaka shirikisho huandaa mafunzo kwa kuangalia mahitaji ya Sekta ya Madini. Alisema vyuo vilivyosajiliwa vitanufaika kutumia fursa hiyo kwani ni ya kipekee.
Aliongeza kwamba Sekta ya Nishati na Madini inahitaji kufikia lengo la kuchangia katika pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, kwa kuwa kwa miaka iliyopita ni asilimia tatu pekee inayotoka katika sekta hiyo.
Alisema kutokana na kufungiwa kwa Mgodi wa Geita na Kilawaka mapato hayo yamezidi kupungua kutokana na kutokuwepo kwa nguvu kazi ya kutosha.

No comments: