MAWAZIRI WA SADC WAKUTANA KUJADILI UGONJWA WA EBOLA


Mawaziri wa  Afya na wadau wengine wa afya wa nchi  wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika  (SADC), leo wanakutana kwenye mkutano wa dharura kuzungumzia hatua za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Mkutano huo unafanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini  una lengo la kutoka na maazimio ya pamoja ya jinsi ya kukabili  mlipuko wa ugonjwa huo ulioenea Magharibi mwa Afrika ambao umeua mamia ya watu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki mkutano huo ikiwakilishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Steven Kebwe ambaye ameshawasili nchini humo.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja alisema  Naibu Waziri atakaporejea nchini, atatoa taarifa ya yaliyojiri na hatua walizoafikiana kuchukua kuthibiti ugonjwa huo.
“Ni kweli kuna mkutano huo, na sisi kama wanachama wa SADC, tunahudhuria, Naibu Waziri tayari yupo huko akirejea tutautaarifu umma yaliyojiri,” alisema Mwamwaja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sekretarieti ya SADC, mkutano huo wa dharura, unafanyika leo jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Shirika la Afya Duniani (WHO), na wadau wengine wanashiriki.
“Lengo la mkutano huo ni kuja na nguvu ya pamoja ya nini cha kufanya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo, ambao unaendelea kuangamiza maisha ya watu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema mkutano huo, utatoka pia na maazimio ya pamoja ya mawaziri  hao jinsi ya kudhibiti ukanda wa SADC, dhidi ya ugonjwa huo.
Ugonjwa huo usio na tiba wala chanjo hadi sasa umekumba nchi za Guinea, Liberia, Sierre Leone na Nigeria. Umesababisha vifo vya zaidi ya watu 800 wakiwemo pia wataalamu na watafiti wa ugonjwa huo.
Hivi karibuni, serikali ilitoa hadhari kuhusu ugonjwa huo na kusema imesambaza wataalamu wake kwenye mipaka nchi nzima kuukabili endapo utaibuka.
Alisema wataalamu wa afya wataendelea kutoa elimu ya afya juu ya ugonjwa huo ambao haujaripotiwa kuingia nchini.
Dalili za ugonjwa wa Ebola ni pamoja na homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na kupatwa na vidonda kooni.
Baada ya dalili hizo mgonjwa hutapika, kuharisha, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na vipele mwilini na kutokwa na damu sehemu zote mwilini zenye matundu na mwisho ni kifo.
Dalili hizo huonekana baada ya siku mbili hadi 21, ya mtu kupatwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

No comments: