UKAWA PASUA KICHWA, KIKAO CHAFANYIKA MASAA 10 BILA MAFANIKIO

Licha ya agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwataka viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wao, wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya wananchi (UKAWA), kuacha kususa na kurejea katika vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ili kuendelea na mchakato huo, kufikia jana hakukuwa na mwelekeo wa kulegeza msimamo wao.
Hali hiyo inajitokeza, licha ya jana kuwapo kwa kikao kirefu cha maridhiano baina ya pande zinazovutana, Ukawa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mchakato huo, unaotarajiwa kuendelea tena kwa siku 60 kuanzia Jumanne ijayo mjini Dodoma.
Katika nasaha zake kwa Ukawa juzi, wakati akihutubia taifa kupitia utaratibu aliojiwekea wa kuzungumza na wananchi kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete aliahidi kuwa tayari kusaidia kwa lolote pale atakapohitaji. Alisisitiza kuwa lengo lake ni kuona Watanzania wanapata Katiba bora, wanayoihitaji.
Hata hivyo, katika kikao cha maridhiano jana, kilichokuwa cha nne na kilichotarajiwa kuwa cha mwisho ili kupata mwafaka kamili, wajumbe waliokutana kwa zaidi ya saa 10 katika hoteli ya Sea Cliff, Masaki jijini Dar es Salaam chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, msimamo wa Ukawa ulibaki kutorejea bungeni.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho, kilichokuwa na ajenda moja tu ya kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni, kuendelea na mchakato wa Katiba mpya, zinasema hatua hiyo imemkatisha tamaa na kumvunja moyo Jaji Mutungi, huku wajumbe wa CCM wakiwaangushia lawama wenzao kuwa hawaoneshi uzalendo na nia ya kuwapa Watanzania Katiba mpya.
Mmoja wa maofisa kutoka Ofisi Msajili aliyekuwa eneo hilo la hoteli hiyo, lakini alisisitiza kutotajwa jina, alielezea kushangazwa na uamuzi wa Ukawa, akisema kila mara wanapoitwa kwa ajili ya kikao cha kumaliza mvutano baina ya pande mbili, wamekuwa na madai mapya, hali inayochangia ugumu wa kufikia mwafaka.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)  ya CCM wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akizungumza jana kwa njia ya simu, alisema anasikitishwa na kile alichokiita unafiki wa Ukawa katika kufikia mwafaka chini ya upatanishi wa msajili wa vyama nchini.
“Ni aina ya unafiki na nadhani wana kitu cha ziada zaidi ya Katiba, haiwezekani kila siku zitafutwe sababu za kukwepesha mwafaka.  Inaonesha kuwa watu hawana nia njema na dhamira ya Rais Jakaya Kikwete na Watanzania ya kuwa na Katiba mpya…mambo ya ajabu kabisa,” alisema Nnauye.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya ofisi ya Msajili, kikao cha jana kilitarajiwa kuwa kikao cha mwisho cha maridhiano katika juhudi hizo za kukwamua mchakato huo ili kuwapa wajumbe wa Ukawa, ambao pia ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, nafasi ya kujiandaa na safari ya kuelekea Dodoma kwenye vikao vya Bunge hilo vinavyotarajiwa kuanza rasmi Agosti 5, mwaka huu.
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni jana, kulikuwa na taarifa za ndani ya kikao hicho, zinazoeleza wazi kwamba hakukuwa na uwezekano wowote wa pande mbili hizo kufikia maridhiano baada ya Ukawa kuwasilisha hoja zao tisa mpya.
Waliwasilisha hoja hizo mpya, badala ya hoja mbili ambazo ziliridhiwa na pande mbili hizo katika kikao kilichopita, ambacho kilikuwa ni cha tatu, kwamba zingejadiliwa katika kikao jana na kufikia hitimisho la majadiliano hayo.
Kwa mujibu wa habari hizo, hoja tisa hizo zilizowasilishwa na Ukawa katika kikao hicho cha jana, zilishajadiliwa na kufikiwa muafaka na pande mbili hizo katika kikao kilichopita, zikawekwa kiporo hoja mbili, ambazo ndizo zilipaswa kujadiliwa jana kabla ya kufikia hitimisho.
“Hawa Ukawa wanamvuruga tu Msajili kwa sababu hawaeleweki ni kitu gani hasa wanachokitaka…kwa kweli wamem-put off (kuvunja moyo, kuvunja nguvu) Msajili wa vyama vya siasa, uwezekano wa kufikia maafikiano na maridhiano ili tuweze kurejea bungeni kuendelea na mchakato wa kutafuta Katiba mpya ni mdogo sana,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kikao kwa sharti la kutotajwa.
Nje ya kikao hicho, baadhi ya maofisa wa Ofisi ya Msajili, walionesha kushangazwa na hali hiyo ya kutofikia muafaka, wakisema kwa vikao vinne tu hivyo, Ofisi ya Msajili imeingia gharama kubwa kuliko ilivyofikiriwa awali, wakati Jaji Mutungi anapanga mipango ya kuzikutanisha pande mbili hizo.
Kwa mujibu wa maofisa hao, kikao cha kwanza cha pande mbili hizo za Ukawa na CCM, kilichofanyika chini ya upatanishi wa Jaji Mutungi, kiliwakutanisha wenyeviti na makatibu wakuu wa vyama vinne vya siasa vya CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na hivyo kikao hicho kuwa na wajumbe tisa akiwemo mpatanishi, Msajili wa vyama.
Katika kikao hicho cha kwanza, habari zinasema Ukawa waliomba kupanua wigo kwa kuongeza idadi ya wajumbe zaidi ili kila upande uwe na wawakilishi 20, kwa maana ya Ukawa wawe na wajumbe 20 na CCM wawe na wajumbe 20.
Habari zinasema, busara ya Msajili wa vyama na wajumbe wengine wa kikao hicho, wazo hilo la Ukawa lilikubalika na hivyo kikao cha pili, cha tatu na hicho cha jana vikawa vinahudhuriwa na wajumbe 41, kwa maana ya Ukawa 20, CCM 20 na Msajili wa vyama.
Idadi hiyo ya wajumbe na mahali vinavyofanyikia vikao hivyo, hoteli ya Sea Cliff, kuanzia ukumbi na huduma nyingine za hoteli, ikiwemo chakula na vinywaji ndivyo vinavyodaiwa kuongeza gharama ambayo awali Ofisi ya Msajili haikuwa imezifikiria.
Kutokana na kuwepo kwa dalili za kukosekana kwa mwafaka baina ya pande hizo, jana gazeti hili lilifanya juhudi za kuwasiliana kwa nyakati tofauti na viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR), lakini kwa muda mrefu siku zao za viganjani ziliita bila kupokelewa.
Hata hivyo, juzi viongozi wa Ukawa walikutana katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CUF Buguruni jijini Dar es Salaam na kutoa tamko la kutorejea kwenye Bunge Maalum la Katiba kuendelea na vikao, wakisema ni muujiza tu ndio unaoweza kuwafanya warejee.
Wajumbe wa Ukawa walisusia vikao vya Bunge Maalumu katika siku za mwisho za awamu ya kwanza ya bunge hilo lililoketi kwa siku 70 kuanzia Februari 11 mwaka huu, kwa kile alichodaiwa wanaburuzwa na wenzao wa CCM, ambao kimsingi ndio wengi, kutokana na uwakilishi wao katika Bunge la Muungano, ambalo wajumbe wake wameunganisha na wengine 201 walioteuliwa na Rais hivyo kuunda Bunge Maalumu la Katiba.

No comments: