MAMA WA MTOTO WA MIEZI 10 NAYE KORTINI KWA MABOMU ARUSHA

Watuhumiwa 19 wa ulipuaji mabomu mkoani Arusha, jana walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Walisomewa mashtaka yanayowakabili chini ya ulinzi mkali ndani na nje ya viwanja vya mahakama.
Wakati hayo yakitokea mjini Arusha, jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, Shekhe Farid Hadi Ahmed (45) na mwenzake, Jamal Swaleh wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi.
Mjini Arusha, ulinzi uliimarishwa kwa kila aliyeonekana maeneo hayo kuanzia mapema asubuhi.
Walioingia mahakamani walikaguliwa kwa vifaa maalumu vya ukaguzi pamoja na  askari polisi wenye silaha na mbwa.
Ilipotimu saa 5:00 asubuhi, pikipiki ya polisi iliyokuwa ikipiga king’ora, iliongoza msafara wa magari matatu, yaliyobeba washitakiwa.
Baada ya saa mbili baadaye, watuhumiwa hao akiwemo Sumaiya Ally (19), mama mwenye mtoto mwenye umri wa miezi 10, walishushwa ndani ya magari na kuingizwa chumba cha mahabusu, kusubiri kusomewa kesi yao.
Waliingizwa chumba cha mahakama saa 8.00 mchana na kusomewa mashitaka yanayowakabili mbele ya mawakili wa Serikali, Augustino Kombe, Felix Kwetukia na Marceline Mwamunyange.
Wakili Kwetukia alisoma shitaka la kwanza  kwa kudai linawahusu watuhumiwa Yahaya Mpemba (37), Yusuph Huta (30), Kassim Ramadhan (34), Jafari Lema (38), Abdul Humud `Wagoba’ (30), Said Temba (42), Idd Yusuph (23), Hassan Mfinanga (57), Anwar Hayel (29), Nabian Mswahili na Yusuph Ramadhan (23).
Alidai washitakiwa hao kwa pamoja, kati ya Januari na Februari mwaka huu Jijini Arusha, walikula njama ya kufanya vitendo vya ugaidi nyumbani kwa Shekhe Sudi Ally Sudi.
Pia, alidai shitaka la pili linahusu watuhumiwa wote hao,  kwamba Julai 3 mwaka huu, eneo la Majengo Chini walifanya kitendo cha kigaidi na kurusha bomu nyumbani kwa Shekhe Sudi na kumsababishia majeraha.
Alidai shitaka la tatu, linawahusu washtakiwa hao  la kufanya vitendo vya kigaidi kwa kurusha bomu la kutupwa kwa mkono na kusababisha kifo.
Shitaka lingine linawakabili washtakiwa Yahaya Twahir (37), Lema  na Humud ambao ilidaiwa kuwa  kati ya Juni na Julai mwaka huu, katika siku tofauti kwa pamoja walitoa fedha kwa ajili ya kufanya tukio la ugaidi. Hawakutakiwa kujibu lolote.
Katika kesi nyingine inawakabili Huta, Lema, Ramadhan, Humud, Abashar Omar (24), Morris Muzi (44), Niganya Niganya(28), Baraka Bilango (40), Abdulrahman Hassan (41), Said Temba (42) ambao kwa pamoja walisomewa shtaka la mauaji. Walidaiwa kuwa Juni 5 2013 katika Viwanja vya Soweto, walimuua Ramadhan Juma na kuwajeruhi wengine. Tuhuma nyingine inamkabili Huta na wenzake tisa, wanaotuhumiwa kukusanya zana kwa ajili ya ugaidi.
Wakili Kombe alidai  kuwa Lema, Abdul Mohamed, Abdulrahman Hassan, Morris Muzi, Niganya Niganya na Baraka Bilango  kwa pamoja kati ya Juni 23 na Julai 21 eneo la Ngusero, walikusanya mabomu mawili ya kurusha  kwa mkono kwa lengo la kufanya ugaidi.
Shitaka la pili ni kwa washitakiwa hao hao, kati ya Juni 23 na Julai 22 mwaka huu, wanadaiwa kukusanya mabomu matano kwa nia ya kufanya matukio maovu.
La tatu ni kwa washitakiwa hao kwa pamoja kuwa kati ya Juni 23 na Julai 22 mwaka huu maeneo ya Ngusero, walikusanya risasi sita aina ya Shortgun kwa lengo la kufanya ugaidi.
Shitaka la nne ni kwa mshitakiwa Bilango, Niganya na Muzi ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kusambaza mabomu matano mkoani Kigoma  kwa lengo la kufanya ugaidi.
Shitaka lingine ni kwa washtakiwa Huta, Lema na Ramadhan, ambapo wakili Mwamunyange alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya ugaidi. Ilidaiwa kuwa  Februari 26 mwaka huu ndani ya Jiji la Arusha, kwa pamoja walifanya njama ya kufanya ugaidi msikiti mkuu wa Ijumaa.
Aidha, ilidaiwa watuhumiwa hao kwa pamoja Februari 28 mwaka huu wakiwa katika msikiti wa Ijumaa, walimmwagia usoni tindikali Shekhe Mustapha Kiago na kumsababishia majeraha.
Kosa jingine linahusisha watuhumiwa hao kummwagia tindikali usoni Khalid Mustafa katika msikiti huo Februari 28, mwaka huu. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 15 mwaka huu
Shitaka lingine linamhusu Huta, Lema, Ramadhan Waziri (28), Ramadhan (34) kwa pamoja  Julai 2009 hadi 2013 walifanya njama ya kufanya ugaidi, Kombe alidai  washtakiwa hao Julai 11 mwaka maeneo ya Kwamrombo, walimwagia tindikali Shekhe Said Makamba. Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilka na Hakimu Msofe aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15 mwaka huu.
Shitaka lingine linamhusu Huta, Mustapha Kiago (49) Ramadhan na Abdul-Aziz Mkindi (49). Walidaiwa kuwa kati ya  Oktoba mosi na 25 mwaka 2012 ndani ya Jiji la Arusha,   walifanya njama ya kumdhuru Shekhe Abdulkarim Jonjo
Katika shitaka jingine, Oktoba 25 mwaka huo wa 2012 eneo la Sokoni 1 jijini Arusha, wanatuhumiwa walirusha bomu lililotengenezwa kienyeji na kulipuka kisha kumsababisha majeraha Shekhe Jonjo.
Shitaka la tatu ni kwa washtakiwa hao Huta, Kiago, Ramadhan, Mkindi kwa pamoja wanatuhumiwa kutoa ufadhili ili kufanya matukio ya kigaidi. Uchunguzi wa kesi hiyo, bado unaendelea na kesi imepangwa Agosti 15 mwaka huu.
Shitaka lingine linawahusu Ibrahim Leonard (37), Anwar Hayel (29), Yassin Shaaban (20) ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kwa kosa la kushawishi na kutoa ufadhili ili kufanikisha matendo ya kigaidi. Wanashitakiwa pia kwa kushawishi watu 10 kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Alshabab Islamic maarufu Alshab .
Kwa mujibu wakili Mwamnyange,  vijana walioshawishiwa kujiunga na kikundi hicho ni Abuu Harris, Abuu Shafy, Mwinyi Mwinyi, Abuu Mujahd, Soud Kabaju, Ahmed Ismail, Omary Mohamed, Issa Mkombo, Qassim Salaf na Rashid Salaf
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na baada ya kusomewa mashtaka saba yanayowakabili, walitolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi na askari Magereza kwenda mahabusu ya gereza la Kisongo hadi Agosti 15 mwaka huu, watakapofikishwa tena mahakamani hapo.
Kiongozi wa Uamsho Zanzibar, Shekhe Farid Hadi Ahmed jana alipandishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi sambamba na mwenzake, Jamal Swaleh.
Walisomewa mashitaka manne na mawakili waandamizi wa Serikali, Bernald Kongola, Peter Njike na George Barasa mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema.
Ilidaiwa kati ya Januari mwaka jana na Juni mwaka huu katika maeneo tofauti nchini, washitakiwa hao walikula njama za kuingiza watu nchini kufanya vitendo vya ugaidi.
Wakili Kongola alidai kuwa katika tarehe tofauti nchini, washitakiwa walikubali kuwaingiza nchini watu waliokuwa na lengo la kufanya vitendo vya ugaidi.
Katika mashitaka mengine yanayomkabili kiongozi huyo wa uamsho, ilidaiwa aliwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omar kushiriki katika  vitendo vya kigaidi.
Aidha, anadaiwa katika kipindi hicho, alishiriki na kusaidia kutendeka kwa vitendo vya ugaidi. Washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika na kuomba itajwe Agosti 6 mwaka huu, ambapo watakuwa na ombi.
Hakimu Lema alikubali ombi hilo. Aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6 mwaka huu itakapotajwa tena. Washitakiwa walirudishwa rumande, kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana.

No comments: