SURA ZOTE BUNGE MAALUMU KUJADILIWA BILA KUPIGIWA KURA


Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, amejibu mapigo ya wanaozungumzia mchakato wa Katiba mpya nje ya Bunge Maalumu.
Amesema Bunge hilo lipo kihalali na lina haki ya kujadili na hata kuongeza sura, ili kuifanya Katiba kuwa imara na yenye kujibu matakwa ya wananchi.
Kiongozi huyo wa Bunge Maalumu, alisema hayo jana wakati wa hotuba yake ya ufunguzi, ambayo ilijikita zaidi katika tuhuma  zinazoelekezwa dhidi ya Bunge hilo na kwanini lazima liendelee na mkutano wake.
Alisema kwamba msingi wa majadiliano yote tangu kuanza kwa Bunge hilo, ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema anayekabidhiwa rasimu, ana haki na mamlaka ya kuirekebisha, kwa sababu rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza bila kupata ithibati ya taasisi ya juu zaidi.
“Itakuwa ni jambo la ajabu na lisilo na mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili rasimu, ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati wa kuwasilishwa kwake,” alisema Sitta.
Alisema kutokana na ukweli huo, wale wanaodai kuwa bungeni hapo hawajadili Rasimu ya Katiba, hawasemi ukweli  na badala yake wanapotosha wananchi.
Sitta akihutubia kwa upole, alisema pamoja na kuwa hakupenda kuzungumzia hoja mbalimbali, zinazotawala gumzo ya mchakato wa Katiba mpya nchini, aliwataka watu hao kupunguza jazba, chuki na upotoshaji.
Alitaka Bunge hilo, kusaidiwa kwa mawazo chanya ili limalize kazi zake.
Aliwataka pia wajumbe  waliopo ambao ni zaidi ya robo tatu, kufanyakazi kwa makini, wakijadiliana kiungwana.
Alisema kwamba tofauti za mawazo, zisiwafanye kuingiza chuki na maneno yasiyofaa, kwani wapo katika eneo linalotakiwa la kutunga Katiba ya wananchi.
“Pamoja na uhalali wa kisheria wa Bunge hili Maalumu kuendelea kufanyakazi zake, linao pia uhalali wa kisiasa kutokana na sifa za uwakilishi wetu na pia maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu,” alisema Sitta.
Alisema upo upungufu katika rasimu iliyopo, kwa kuacha masuala ya kuwezesha serikali za mitaa, kutoa maelekezo kuhusu msuala ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine za Taifa.
Sitta alisisitiza kuwa kutokana na ukweli huo, ni lazima wajadili na kuboresha kwa kuyaongeza mambo, ambayo hayapo kwa faida ya Taifa.
Alisema kutokana na maudhui ya rasimu kujikita katika kuimarisha Muungano na kuleta uwiano bora zaidi wa mamlaka za Tanzania Bara, Zanzibar na Muungano, kuimarisha haki za binadamu, kuzuia wachache kufuja rasilimali za Taifa, kutambua haki za ardhi kwa wakulima na wafugaji na kuweka sheria za kuzuia ukandamizaji wa raia, rasimu lazima ijadiliwe.
Aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuendelea na kazi waliyotumwa, kwa kuwa wapo kihalali kisiasa na kisheria.
“Kutofautiana maoni hakuwapi hadhi tofauti baadhi ya wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi mbele ya wananchi na kupotosha ukweli,” alisema.
Rasimu hiyo yenye jumla ya Sura 17, zimepitiwa sura mbili na zimebaki siku 60 za kufanyia kazi, kukamilisha  sura nyingine 15.
Katika hotuba hiyo, pia Sitta alielezea mabadiliko yaliyokusudiwa katika kanuni, kwa lengo la kuzifanya siku 60 zitoshe kukamilisha kazi iliyopangwa.
Katika mabadiliko hayo, wajumbe sasa hawatapigia kura sura mbili, walizokwisha kujadiliwa  mpaka hapo watakapomaliza kujadili  Sura 15 nyingine.
Akiwasilisha bungeni  jana Azimio la Kufanyia Marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalumu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, alitaja kanuni mbalimbali ambazo zitafanyiwa marekebisho kuwa ni ya 14, 15, 32,32B,33, 35,46, 47,54, 60 na 62.
Alisema Kanuni ya 14 inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kufuta Fasili ya 4 ili kuondoa sharti la Bunge Maalumu, kukutana Jumamosi na kwamba hatua hiyo inalenga kuwapa wajumbe muda wa kupumzika na kufanya tafiti na mashauriano juu ya mambo mbalimbali, yanayohusu Rasimu ya Katiba ili kuboresha michango yao wakati wa mjadala kwenye Kamati na ndani ya Bunge Maalumu.
Marekebisho mengine ni Kanuni ya 15 ili kusimamia mahudhurio ya wajumbe kwenye Bunge na Kamati zake.
“Kwa mujibu wa marekebisho haya, kila Mjumbe sasa atatakiwa kusaini yeye binafsi karatasi ya mahudhurio iliyoandaliwa na Katibu wa Bunge Maalumu, kama uthibitisho wa kuhudhuria kwake,” alisema Kificho.
Alieleza kuwa marekebisho mengine ni Kanuni ya 32 Fasili ya Kwanza, inayolenga kuondoa utaratibu uliokuwepo awali wa kila kamati ya bunge hilo, kujadili rasimu kwa wakati mmoja kwa kuzingatia mgawanyo wa sura angalau mbili za rasimu ya Katiba zinazofanana.
“Hivyo inapendekezwa kwamba kila kamati ijadili sura zote za rasimu ya Katiba, aidha katika Fasili ya Pili inapendekezwa muda wa kujadili sura hiyo ambapo kamati zitajadili  sura za rasimu ya Katiba kwa muda usiozidi siku 15.
“Utaratibu unaopendekezwa utafanya sura za rasimu ya Katiba zilizobaki zijadiliwe kwa muda mfupi, lakini kwa ufanisi mkubwa,” alisema.
Kanuni nyingine ni ya 32B, ambayo inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kuifuta na kuandikwa upya kwa lengo la kuruhusu masharti ya Kanuni ya 46 na 46A, yanayohusu Bunge Maalumu juu ya mamlaka ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, kutoa adhabu yatumike pamoja na marekebisho husika, kuendesha majadiliano kwenye Kamati.
Marekebisho mengine ni Kanuni ya 33 inapendekezwa Fasili ya pili ifanyiwe marekebiho kwa kufuta dakika 60 na badala yake iwekwe dakika 120 kwa lengo la kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa  ya maoni ya walio wengi, pia kufuta Fasili ya 5,6 na 7 na kuandikwa upya kwa  kuongeza muda wa kuwasilisha maoni ya wachache kutoka dakika 30 hadi dakika 60.
“Kanuni ya 35 inapendekezwa Fasili ya 6 hadi 11 zifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuweka utaratibu wa namna ya kujadili na kupitisha masharti ya sura za Rasimu ya Katiba pamoja na sura mpya zitakazopendekezwa.
“Mapendekezo hayo yanaaondoa utaratibu wa kujadili na kupitisha angalau  sura mbili za rasimu ya Katiba kwa kamati namba 1 hadi 12 na badala yake inapendekezwa kujadili sura zote za rasimu ya Katiba kwa kila kamati na hatimaye uamuzi kufanyika baada ya mjadala wa sura zote kukamilika,” alisema.
Pia, alieleza kuwa Kanuni ya 36 inapendekezwa ifutwe na kuandikwa upya kwa lengo la kuainisha utaratibu, utakaotumika wakati wa kupigia kura ibara za rasimu ya Katiba.
“Aidha inapendekezwa upigaji kura kwa ibara za sura zote za Rasimu ya Katiba, ufanyike kwa muda usiozidi siku 15,” alisema.
Aliongeza kuwa pia kanuni ya 46 inapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kuongeza fasili mpya ili kumpa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, mamlaka ya kutoa adhabu kwa mjumbe atakayekiuka fasili ya kwanza.

No comments: