WAZIRI WA ZAMANI SMZ AREJESHWA RUMANDE


Aliyekuwa Waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid, amefikishwa mbele ya Mahakama ya Mkoa Vuga, akikabiliwa na makosa matatu na kisha kurejeshwa rumande.
Katika eneo la mahakama hiyo, eneo la Mji Mkongwe, ulinzi uliimarishwa, ambapo askari Polisi walitanda kila kona kuingia katika eneo hilo.
Mansour aliwasili mahakamani hapo saa nane mchana, kusomewa mashitaka yanayomkabili ya kupatikana na silaha kinyume na Kifungu Namba 6 (3) na 34 (1)(2) cha Sheria ya Silaha na Risasi ya 1991 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Sura ya 223.
Kosa la pili aliloshitakiwa ni kupatikana na risasi kinyume na Kifungu  cha 6 (3) na 34 (1) (2) Sheria Namba 7 ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Kosa la tatu ni kupatikana na risasi za bunduki aina ya shot gun kinyume na Kifungu cha 34 (1)(2)  Sheria ya Risasi na Silaha  Namba 2 ya mwaka 1991.
Akimsomea mashitaka hayo mahakamani hapo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Raya Mselem aliyekuwa na msaidizi wake, Maulid Ali alidai kuwa Agosti 2 mwaka huu saa 7:00 mchana huko Chukwani, nyumbani kwa mshitakiwa, alikutwa na na silaha aina ya bastola yenye namba F 76172W, kinyume na sheria.
 Aidha, alidai kuwa mshitakiwa huyo, alikutwa na risasi za moto 295 za bastola, jambo ambalo ni kinyume na sheria, sambamba na kukutwa na risasi 112 za shot gun badala ya 50 alizoruhusiwa pamoja na bunduki aina ya shot gun.
 Mshitakiwa huyo alisomewa mashitaka yake hayo mbele ya Naibu Mrajisi wa Makama Kuu ya Zanzibar, Khamis Ramadhan, ambaye aliamuru mshitakiwa huyo arejeshwe rumande hadi Agosti 18 mwaka huu. 
Wakili wa mshitakiwa huyo, Omar Said Shaaban, aliyekuwa na msaidizi wake, Gaspa Nyika, alidai mahakamani hapo kuwa anatarajia kupeleka ombi la dhamana Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Kabla ya kufukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki na sasa amejiunga na CUF na kutangaza kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

No comments: