SERIKALI YAONGEZA NGUVU KUKABILIANA NA UGONJWA WA EBOLA

Serikali imeongeza nguvu ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa ebola iwapo utatokea, kwa kuwapima wasafiri na wageni wanaoingia nchini kupitia viwanja vikubwa vitano vya ndege.
Vipimo hivyo vitafanywa ili kubaini iwapo wana vimelea vya ugonjwa huo, kwa kutumia mashine za thermoscan  zinazotarajiwa kuingia nchini wiki mbili zijazo.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Dk Kebwe Stephen Kebwe alipokuwa akizungumzia ripoti ya mkutano wa dharura kwa  mawaziri wa Afya na wadau wengine wa afya wa nchi  wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), kuhusu ebola.
Dk Kebwe alisema katika mkutano huo wa dharura uliofanyika Agosti 6, mwaka huu, Afrika Kusini, ulimalizika kwa kuwekeana malengo na maazimio ya kutekeleza kwa haraka ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo, ambao umeathiri zaidi nchi za Afrika Magharibi.
“Tumekubaliana jambo ili liwe nyeti na tunachukua hatua za haraka kuudhibiti na kuwaelimisha wananchi, mlipuko wa kipindi hiki ni mkubwa, haujawahi kutokea duniani”, alisema Dk Kebwe.
Alisema ugonjwa huo usio na tiba wala chanjo hadi sasa umeshazikumba nchi za Guinea, Liberia, Sierre Leone na Nigeria na umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000, wakiwemo pia wataalamu na watafiti wa ugonjwa huo.
Pia umezikumba nchi za Mashariki ya Kati, ikiwemo Saudia Arabia na Falme za Kiarabu kwenye mji wa Dubai.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Tanzania kukabiliana na ugonjwa huo, Dk Kebwe alisema wiki mbili zijazo, mashine za thermoscan  zilizoagizwa kutoka Afrika Kusini zitawasili nchini na kusambazwa kwenye viwanja vitano vya ndege.
Viwanja hivyo ni pamoja na cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), cha Kilimanjaro (KIA), wa Mwanza, Zanzibar na Mbeya.
Alisema mashine hizo zitakuwa zikiwapima wasafiri na wageni wote wanaoingia nchini kutokea nchi za Afrika Magharibi na kwengineko, ili kubaini kama wana vimelea vya ugonjwa huo, ili iwe rahisi kutibu na kuepusha maambukizi kwa wengine.
“Ugonjwa huu hauna kinga wala chanjo na unasambaa kwa haraka sana, hivyo kama tutabaini wenye vimelea au ugonjwa huo mapema, tunaweza kuwatibu kwa maradhi ya awali na kuepusha kuambukiza wengine,”alisema Dk Kebwe.
Alisema serikali kwa kutambua uzito wa ugonjwa huo, umechukua hatua za haraka kwa kupeleka wataalamu wa afya 17,000 kwenye mipaka yote nchini pamoja na vifaa tiba kama vile dawa, buti, miwani, maski, aproni pamoja na nguo za kujikinga.
Aidha, msambazaji wa vifaa hivyo ana taarifa na iwapo vitahitajika vingine ndani ya saa 48 hadi 72, vifaa hivyo vitakuwa vimeshaagizwa nje ya nchi na kuingia.
Ingawa ugonjwa huo haujaingia nchini, Dk Kebwe alitoa mwito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kutoa taarifa na kwenda kwenye kituo cha afya iwapo wataona dalili za ugonjwa huo, ambazo ni pamoja na homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kumwa kichwa na kupatwa na vidonda kooni.
Baada ya dalili hizo, mgonjwa hutapika, kuharisha, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na vipele mwilini na kutokwa na damu sehemu zote mwilini zenye matundu na mwisho ni kifo. Na kwamba dalili hizo huonekana baada ya siku mbili hadi 21, ya mtu kupatwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

No comments: