MKE APANDISHWA KORTINI KWA KUMFANYIA FUJO MUMEWE

Mkazi wa eneo la Majengo mjini Singida, Anna Bonaventure (34) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Utemini, akikabiliwa na mashitaka ya kumfanyia fujo mumewe, Abdallah Ally (34) kwenye eneo lake la biashara.
Ilidaiwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ferdinand Njau kuwa Julai 22 mwaka huu saa 11.30 jioni katika eneo la Mwenge mjini Singida, kwa makusudi Anna alifanya fujo kwenye meza ya biashara ya Abdallah huku akijua wazi kuwa  kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Aidha, ilidaiwa kuwa fujo hiyo ilisababisha wateja wa Abdallah kuondoka bila kununua bidhaa yoyote zikiwemo mboga za majani.
Kutokana na kitendo hicho, amani na utulivu vilitoweka kwa muda hadi mshitakiwa alipoondolewa kwa nguvu eneo la tukio.
Mlalamikaji Abdallah, ambaye ni mlemavu wa  miguu, aliiambia mahakama hiyo kuwa mke wake Anna amemchosha kwa vitendo vyake vya fujo vinavyochangiwa na ulevi uliopindukia.
“Fujo za mke wangu pia zimekuwa zikichangia tufukuzwe mara kwa mara kwenye nyumba tunazopanga kwa ajili ya kuishi. Huyu mke wangu ni mlevi mkubwa wa pombe za kila aina na mara nyingi amekuwa akilala nje,” adai Abdallah na kuongeza:
“Hii mimba unayomwona nayo nadhani sio yangu, atakuwa amepewa na walevi wenzake kilabuni".
Mshitakiwa Anna, ambaye wakati huo alikuwa amezungukwa kizimbani na watoto wake watatu wenye umri chini ya miaka mitano alikiri kunywa pombe na pia kulala nje ya nyumba yao kwa kusema: “Mume wangu nakupenda sana kuanzia leo, nakuahidi naacha kabisa kunywa pombe na wala sitalala tena nje ya nyumba yetu".
Anna alidai kuwa mara nyingi mume wake amekuwa akimnyonga shingo na kumpiga kwa kutumia magongo yake ya kutembelea lakini vitendo hivyo havijaathiri penzi lake kwa mumewe.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa tena Agosti 11 mwaka huu na mshitakiwa amejidhamini kwa ahadi ya maandishi ya Sh 500,000.

No comments: