TMA YAASA WAKULIMA KUZINGATIA HALI YA HEWA

Wakulima nchini wametakiwa kutumia taarifa za hali ya hewa ili kuwa na uhakika wa kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara na kuepuka kulima kwa mazoea kunakowasababishia kupata hasara wakati wa mavuno.
Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi wakati wa wiki ya Maonesho ya Wakulima (Nanenane) ya Kanda ya Mashariki katika  viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage, mjini Morogoro.
Maonesho hayo kilele chake kilikuwa juzi ambapo katika Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro yalifungwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Dk Kijazi alisema hakuna kilimo bora bila kufuata mbinu bora ikiwemo taarifa za hali ya hewa zitakazomsaidia mkulima kupanga mipango yake ya uendeshaji wa kilimo cha mazao mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa mkoa wa  Pwani, Mwantumu Mahiza  aliwataka vijana kutumia fursa zilizopo za  kilimo na ufugaji ili kuweza kupata manufaa ya kimaendeleo kulingana na lengo walilokusudia.
Mwantumu aliwasihi vijana kuacha kudanganywa na wanasiasa wasio na nia njema kwa taifa, ambao wanaotumia kigezo cha ajira kama ajenda kuu bila kuwaelekeza fursa zilizopo na kuwapa miongozo ya kujishughulisha na kazi.

No comments: