MFUMUKO WA BEI WAONGEZEKA KIDOGO

Ofisa ya Takwimu ya Taifa (NBS) imesema mfumko wa bei wa mwezi Julai, umeongezeka kidogo kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa Juni hadi  asilimia 6.5.
Hata hivyo, alisema  bei za bidhaa za vyakula, hazikupanda licha ya kuwepo malalamiko kutoka kwa wananchi, kuwa bei za vyakula zilipanda maradufu mwezi uliopita.
Mwezi uliopita Waislamu ambao walikuwa kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, walilalamikia kupanda kwa bei za vyakula, hasa wanavyotumia kupika futari kama magimbi, muhogo, viazi, maharage na tambi, kuwa bei yake ilipanda maradufu.
Lakini, NBS imesisitiza kuwa vyakula vinavyotumiwa na Watanzania wengi, bei zake hazikupanda, bali bei za vyakula ambavyo havitumiwi na watu wengi, ndivyo bei yake ilipanda, lakini haikuathiri ukokotoaji wa mfumuko wa bei.
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa NBS, Ephrahim Kwesigabo  alisema jana kuwa kupanda kwa mfumuko wa bei mwezi Julai, kunamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Julai, imeongezeka kidogo, ikilinganishwa na mwezi ulioshia Juni.
"Ila mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi, umebaki kuwa asilimia 8.1 mwei Julai kama ilivyokuwa mwezi Juni," alisema Kwesigabo wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Akizungumzia mfumko wa bei kwa bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula, Kwesigabo alisema badiliko la fahirisi za bei za bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani, limepungua hadi asilimia 7.9 mwezi Julai kutoka asilimia 8.7 mwezi Juni.
Alisema fahirisi za bei kwa bidhaa zisizo za vyakula, limeongezeka hadi asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 mwezi Juni. Alitaja bidhaa hizo kuwa ni bia bei imepanda kwa asilimia 4.4, sigara asilimia 2.1, kodi ya pango asilimia 2.5 na mkaa asilimia 1.2.
Alisema mfumuko wa bei, ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwezi Julai, umepungua hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 3.5 ilivyokuwa Juni.
Kuhusu thamani ya Shilingi ya Tanzania  kwa mwezi Julai, alisema uwezo wa Shilingi 100 katika kununua bidhaa na huduma, umefikia asilimia 67 na senti 04.
Akizungumza mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi, Kwesigabo alisema umeongezeka kwa asilimia 0.1, ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.6 kama ilivyokuwa Juni. Lakini alisema fahirisi za bei, zimeongezeka hadi 149.16 Julai kutoka 148.98 mwezi Juni.

No comments: