Kiwanda cha saruji cha Kampuni ya Dangote, kinachojengwa mkoani Mtwara kinatarajia kukamilika ujenzi
wake na kuanza uzalishaji wa saruji mwishoni mwa mwaka 2015, ambapo mwekezaji
wake, raia wa Nigeria, Aliko Dangote,
amesema kiwanda hicho kitakuwa moja ya viwanda bora duniani.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo iliyotolewa mapema wiki hii,
ujenzi wa kiwanda hicho nchini ni moja
ya miradi ya uwekezaji wa kampuni za
Dangote barani Afrika, unaolenga kuinua uchumi wa nchi hizo na kuboresha maisha
ya wananchi wake.
Ripoti hiyo inasema Kampuni ya Dangote, imepanga kuwekeza kwenye
miradi mipya ya viwanda vya saruji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni
3.9 na kwamba kwa miradi ya viwanda vya saruji kwa Afrika Mashariki, ikiwemo
Tanzania, kampuni hiyo imewekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 600.
Dangote alisema hadi hivi sasa ujenzi wa kiwanda hicho cha saruji
nchini, umekamilika kwa asilimia 25, na hadi mwisho wa mwaka ujao, ujenzi huo
utakuwa umekamilika na kuanza uzalishaji wa saruji.
Alisema kiwanda hicho, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni
tatu za metriki za saruji kwa mwaka.
Mbali na ujenzi wa kiwanda cha saruji nchini, rais huyo alisema
kampuni yake pia imepanga kuwekeza kwenye viwanda vingine vya uzalishaji saruji
barani Afrika kwenye nchi 16.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni hiyo imejipanga kwa miaka
ijayo, kuwekeza zaidi kwenye nchi
mbalimbali na kujenga viwanda bora vya saruji, ambapo kwenye mipango yao
watawekeza pia kwenye nchi za Senegal na
Afrika Kusini.
Akizungumzia jinsi ya kukuza uchumi wa Bara la Afrika, Dangote
alisema ili kuinua uchumi wa Afrika ni lazima ujenzi wa viwanda vyenye
ushindani na mataifa mengine, uwepo ili kuchochea uchumi, hivyo uwekezaji wa
saruji utafanywa pia kwenye nchi za Zambia, Ethiopia, Cameroon na Sierra Leone.
No comments:
Post a Comment