Hatima ya washitakiwa wawili wa kesi ya wizi wa Sh bilioni sita za
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), itajulikana
Oktoba 8 mwaka huu wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itakapotoa uamuzi
kama wana kesi ya kujibu au la.
Endapo Mahakama itawaona washitakiwa
katika kesi hiyo Johnson Lukaza na ndugu yake, Mwesiga Lukaza, wana kesi ya
kujibu watapanda kizimbani kuanza kujitetea, kama hawatakuwa na kesi ya kujibu
wataachiwa huru.
Washitakiwa hao wanadaiwa kati ya mwaka 2004/2005 walikula njama
za kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia Sh bilioni sita kwa udanganyifu
wakidai Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex Ltd ya Tanzania imepewa
mamlaka ya kukusanya madeni ya Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.
Hakimu Mkazi Edson Mkasimongwa alitoa tarehe hiyo baada ya upande
wa jamhuri kufunga ushahidi wao wa mashahidi saba pamoja na vielelezo
walivyowasilisha mahakamani.
Awali, shahidi wa mwisho wa Jamhuri, Ofisa wa Polisi kutoka Kenya
Tom Olanga alidai kuwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Marubeni Corporation
ya Kenya, Hisao Ikegai alikana kuifahamu Kampuni ya Changanyikeni Residential
Complex.
Alidai kuwa, alimhoji Ikegai na alimuonesha hati ya makubaliano ya
kukusanya deni kutoka kampuni hiyo kwenda kampuni ya kina Lukaza, hata hivyo
alidai nyaraka hiyo siyo halali kwa kuwa iliandikwa cheo cha Mkurugenzi ambacho
hawatumii kwenye kampuni yao.
Aidha, alidai hawamfahamu Mkurugenzi Nakasomi Nsuko ambaye
alisaini katika hati hiyo kwa niaba ya kampuni yao na hajawahi kufanyakazi
katika kampuni hiyo, pia hawana kumbukumbu yoyote ya kuwa na deni Tanzania wala
kutoa mamlaka kwa kampuni yoyote kukusanya madeni yao.
Tom alidai katika maelezo yake, Ikegai alidai kwa mujibu wa taratibu zao za kuhamisha fedha
Kampuni ya Japan, lazima iwape taarifa kwa kuwa wao ndiyo wawakilishi wa Afrika
Mashariki na hawawezi kuhamisha fedha bila kupata nguvu ya kisheria kutoka
Japan.
No comments:
Post a Comment