JIJI, WAFANYABIASHARA WAZIKA TOFAUTI ZAO MWANZA


Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza umesema kuwa umeumaliza mgomo wa takribani siku tatu ambao umekuwa ukifanywa na wafanyabiashara wa kati jijini hapa. 
Akizungumza juzi, Mkurugenzi wa jiji Hassan Hida alisema kuwa kimsingi karibu madai yote yaliyoelekezwa kwa jiji na wafanyabiashara hao yametatuliwa. 
“Tulikutana na Jumuiya ya wafanyabiashara na nafurahi kuwaeleza kuwa tulifanya mazungumzo ya kina na wao, na ule mgomo waliokuwa nao, jana kwa ahadi yao wenyewe wamesema mgomo hautaendelea kuwepo”, alisema. 
Alisema hatua hiyo ya makubaliano iliwezesha pande mbili kufikia muafaka kwa mambo ya msingi ambayo yalisababisha wafanyabiashara hao kuingia kwenye mgomo huo na hivyo kushindwa kufungua biashara zao kwa muda wa siku mbili mfululizo. 
“Walituletea madai yao manne ambayo kimsingi walitaka tuyafanyie marekebisho, zikiwemo hoja za utozwaji wa ada za leseni zisizokuwa na kiwango maalumu, upandishwaji wa kodi kwa bidhaa zinapoingia dukani na zinapotoka kwenda kwa wateja baada ya kununuliwa na upandishwaji wa kodi za taka”, alisema. 
Aliyataja madai mengine yaliyotolewa na jumuiya hiyo ya wafanyabiashara kuwa ni pamoja na kile walichokieleza kuwa ni unyang’anyi wa bidhaa zao wakati zinapokuwa zikipakuliwa kwenye magari makubwa yanayoingia madukani, wakishinikizwa na uongozi wa jiji kuwa wanafanyia biashara zao nje, hali ambayo ilielezwa na uongozi wa jiji kuwa wamekuwa wakitumia mfumo huo kukwepa kulipa ushuru wa halmashauri. 
“Hivyo walikuja na mapendekezo ya kunishawishi nitoe tamko juu ya kufuta kodi za uzoaji taka, maegesho ya magari, uingizaji bidhaa madukani na walileta hoja ya kunyang’anywa bidhaa zao pindi zinapokuwa zikipakuliwa na kuingizwa kwenye maduka yao hoja ambazo kimsingi tulizijadili kwa pamoja na kukubaliana”, alifafanua.

No comments: