BODI YA MAGAVANA WA BENKI KUKUTANA

Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa 30 wa mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki (BOG) utakaofanyikia jijini Dar es Salaam, mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa jana jijini hapa na Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha Dk Servacius Likwelile (pichani) na Rais wa Benki ya PTA, kwa vyombo vya habari, mkutano huo utakuwa wa siku moja na utafanyika Agosti 22.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa lengo la mkutano huo ni  kujadili masuala mbalimbali ya kibenki, ikiwemo mpango mkakati wa benki hizo na masuala ya fedha na uchumi kwa nchi washirika.
Wajumbe wa mkutano huo ni Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa nchi washirika ambao ndio chombo cha juu cha ngazi ya maamuzi ya benki katika nchi zao.
Aidha, taarifa hiyo imeongeza  kuwa mkutano huo utatanguliwa na semina ya wafanyabiashara itakayofanyika siku moja kabla ya mkutano mkuu wa magavana hao.
Benki ya PTA ilianzishwa mwaka 1985 ikiwa na jumla ya washirika 22 ikiwemo nchi 18 ambazo ni Burundi, Comoro, Djibouti, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Misri, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Tanzania.
Aidha, PTA inashirikiana na nchi nyingine nje ya bara la Afrika ambazo ni Belarus na China.
Washirika wengine ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Kampuni ya Bima ya Mauritius iitwayo Eagle na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Mauritius.

No comments: