SUNGUSUNGU WADAIWA KUUA WANAKIJIJI WAWILI

Watu wawili wakazi wa Kata ya Ipande – Itigi, wilayani hapa, mkoani Singida wamekufa papo hapo baada ya kupigwa na kisha kuchomwa moto na watu waliojitambulisha kuwa ni sungusungu.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Augustino Raphael aliwataja waliouawa kuwa ni Lameck Joshua (31), mkazi wa kijiji cha Damwelu na Doto Kidai (20) aliyedaiwa kutokea mkoa wa Mbeya.
Raphael alisema kuwa tukio hilo ni la Agosti 07, mwaka huu saa 6 usiku katika kijiji hicho ambapo kundi la watu wapatao 40 waliojitambulisha kuwa ni sungusungu walifika nyumbani kwa Lameck, waligonga mlango wafunguliwe lakini Lameck aligoma kufungua.
Hata hivyo inadaiwa kuwa baada ya kugomewa, kundi hilo lilimtishia Lameck  kuwa asipofungua  wangeiteketeza nyumba hiyo kwa moto baada ya kuimwagia petroli.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya tishio hilo, Lameck alilazimika kufungua mlango na kutoka nje ambapo alikamatwa, akafungwa macho kwa kitambaa kisha akapelekwa kwenye vichaka vya jirani ambapo alipigwa hadi kufa na hatimaye akachomwa moto.
Alisema baada ya tukio hilo, watu hao walienda nyumbani kwa Mapalala na kumkamata Doto Kidai na kumfanyia kama Lameck. Alidai habari zilizoenea kijijini hapo ni kwamba watu waliouawa wanadaiwa kuwa ni wezi wa mifugo.
Akizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Manyoni Magharibi, John Lwanji (pichani) alilaani vikali mauaji hayo kwa vile wauaji walijichukulia sheria mkononi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

No comments: