ALIYEMBAKA MTOTO WAKE WA KAMBO ATIWA MBARONI

Watu watano wanashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani Muleba mkoani Kagera kwa tuhuma mbili tofauti, akiwamo aliyembaka mtoto wake wa kambo.
  Kamanda wa Polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe alisema tukio la kwanza ni la Agosti 4, mwaka huu saa 4:00 usiku katika kijiji cha Buyango kata ya  Buhangaza wilayani humo, ambapo watu wanane walimvamia Buberwa Thomas (42) na kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufa.
Inadaiwa kuwa chanzo cha kifo hicho ni wivu wa kimapenzi, ambapo Buberwa  alikuwa na uhusiano wa mapenzi na Elieth John (17), mkazi wa kijiji hicho wakati huo huo, pia alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na kijana mwingine, Rodgers Evarista (18) ambaye anadaiwa alikuwa mpenzi wake wa siku nyingi.
Watuhumiwa hao wanaoshikiliwa na jeshi hilo mpaka sasa ni Rodgers Evarist (18), anayedaiwa kuandaa mpango mzima wa mauaji, Jovin John (18), Rodgers Gosbert (18) na Enock  Deogratias (17), wote wakazi wa kijiji cha Buyango wilayani Muleba. 
Jeshi hilo linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanne ili waunganishwe na wenzao na wafikishwe mahakamani baada ya upelelezi kukamilika. 
Alisema Rodgers Evarist anatuhumiwa kwa makosa mawili ya  kubaka na kulawiti mtoto, kwani msichana aliyekuwa akifanya naye mapenzi bado ni mtoto kisheria. Pia anatuhumiwa kwa kosa la mauaji. 
Wakati huo huo,  mwalimu  wa madrasa, Fahad Abdulmajid (30) anashikiliwa na jeshi la Polisi kwa kosa la kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kambo wa kike, mwenye umri wa miaka 11. Tukio hilo limetokea katika tarafa ya Nshamba wilayani Muleba. 
Mwaibambe alidai binti huyo alikuwa anaishi na mtu huyo, ambaye ni baba yake wa kambo  wakati mama mzazi wa mtoto huyo, alikuwa amekwenda kwao Tanga. 
Alidai binti huyo baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo, alitoa malalamiko kwa majirani, ambao walitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na kisha taarifa zilipelekwa katika kituo cha polisi cha wilaya ya Muleba. 
Binti huyo alipelekwa katika hospitali ya wilaya kwa ajili ya uchunguzi wa madaktari, ambao  walibaini alikuwa ameharibika sehemu zake za siri kwa kubakwa na kulawitiwa. Baadaye polisi walimkamata mtuhumiwa huyo na atafikishwa mahakamani muda wowote.

No comments: