MANISPAA TEMEKE YATOA MITAJI KWA WENYE VIRUSI 150

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imetoa mitaji ya Sh milioni 50 kwa wananchi 150 waishio na virusi vya Ukimwi baada ya kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na Benki za Maendeleo Vijijini (VICOBA) ili waweze kujiongezea kipato.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na Vijana wa Manispaa hiyo, John Bwana alisema mitaji hiyo ilitolewa kwa mwaka wa fedha 2013/2014. 
“Ukimwi ni janga la kitaifa hivyo tumeendelea kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi na ushauri nasaha, mkazo ukiwa ni kuwashawishi wananchi wapime afya zao kwa hiari,” alisema.
Aidha, alisema vijana 150 waliopo katika makundi maalumu kutoka kata 30, walipatiwa mafunzo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi na stadi za maisha.
Pia,  mafunzo juu ya matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs), yalitolewa kwa watu 180 wanaoishi na virusi vya Ukimwi. 
Alisema Sh milioni 32 zimetumika katika kuwapatia lishe watu 300 wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili kuboresha afya zao.
Bwana alisema kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu, watu 13,720 walijitokeza kupima virusi vya Ukimwi kwa hiari, ambapo kati yao wanaume ni 6,939 na wanawake 6,782. 
Alisema katika idadi hiyo, watu 1,343 walipatikana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, wanaume ni 601 na wanawake 724, ambayo ni sawa na asilimia 9.8 ya maambukizi ya watu waliojitokeza kwa hiari.

No comments: