AELEZA MKE WA KIGOGO TANESCO ALIVYOPATA ZABUNI

Kaimu Meneja Mwandamizi wa Ununuzi wa Shirika la Umeme (Tanesco) Makao makuu, Atanaz Kalikamwe ameieleza mahakama jinsi mke wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa shirika hilo, William Mhando alivyopata zabuni ya usambazaji wa vifaa.
Kalikamwe alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili Mhando, mkewe Eva Mhando na wenzake.
Mhando anadaiwa kutumia vibaya madaraka kwa kutoa zabuni ya usambazi wa vifaa vya ofisini Tanesco kwa Kampuni ya Santa Clara Supplies Company Limited, inayomilikiwa na mkewe na watoto wake.
Mbali na Mhando na mkewe  washitakiwa wengine katika kesi hiyo  wafanyakazi watatu wa zamani wa Tanesco, France Mchalange, Sophia Misida na Naftali Kisinga.
Akiongozwa na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonald Swai, Kalikamwe alidai anakumbuka walikuwa na uhitaji wa vifaa, hivyo walifanya mchakato wa kupata mahitaji kutoka idara husika kisha waliandaa taarifa kwenda katika bodi ya Zabuni.
Alidai bodi ilikubali ununuzi ufanyike hivyo zabuni ilitangazwa katika gazeti na baadaye ilifunguliwa ambapo kulikuwa na washindani wengi wa zabuni hiyo.
Alidai timu ya tathimini iliundwa na kufanya kazi kisha ikapeleka ripoti bodi ya zabuni ambayo ilitoa kibali baadhi ya wazabuni wapewa zabuni hiyo ambapo  kampuni ya Santa Clara ilipewa zabuni katika timu ambayo wajumbe wake walikuwa Mchalange, Kisinga na Sophia ambao ni washitakiwa.
Baada ya kushinda zabuni, wahusika  walitengeneza mkataba na kupeleka kitengo cha sheria ambapo kampuni ya Saint Clara iliyokuwa inawakilishwa na Eva ilisaini mkataba mbele ya Mhando.
Shahidi huyo aliomba kutoa nakala za nyaraka za kuomba kibali cha kutoa tangazo kuhusu zabuni, hata hivyo upande wa utetezi ulipinga kwa madai ni nakala na siyo nyaraka halisi.
Hakimu Frank Moshi aliutaka upande wa mashitaka kuwasilisha nyaraka halisi za kielelezo hicho na kuahirisha kesi hadi Septemba 30 na Oktoba Mosi mwaka huu kesi itakapotajwa kwaajili ya kuendelea kusikilizwa.

No comments: