WENYE DIGRII SASA KUFUNDISHA SHULE ZA MSINGI

Rais Jakaya Kikwete amesisitiza nia ya Serikali kutumia wahitimu wake wa vyuo vikuu, kufundisha shule za msingi huku akiwaweka sawa kwa kuwaambia kufanya hivyo si kuwashushia hadhi.
Hatua hiyo ya walimu wenye Shahada kuanza kufundisha shule za msingi  tofauti na ilivyozoeleka, chini ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, ni sehemu ya mageuzi makubwa, yanayotarajiwa kufanyika  katika sekta ya elimu nchini.
 Rais Kikwete alishawahi kutamka mpango huo wa kutumia wasomi wa vyuo vikuu katika shule za msingi, kutokana na idadi kubwa ya wahitimu wa ualimu, kutarajiwa kuwa kwenye soko la ajira.
Alisisitiza kuwa baada ya mwaka, wahitimu wa vyuo vikuu watafundisha katika shule hizo na kwamba kufanya hivyo si kuwashushia hadhi.
 Akihutubia wananchi mjini Mbinga, kabla ya kufungua kituo cha mabasi na barabara ya Peramiho- Mbinga yenye urefu wa kilometa 78, Kikwete alisema barani Ulaya, hata walimu wa shule za chekechekea wana Shahada na kwamba  hicho ni kipimo cha maendeleo.
Kwa utaratibu uliozoeleka chini ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, walimu wa shule za msingi ni wenye cheti. Hata hivyo, kulingana na taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wapo wanaochukua Shahada, wanaosomea kufundisha elimu ya msingi.
“Wakati umebadilika…leo utamchukua Standard Seven ( Darasa za Saba) kwenda chuo cha ualimu? Leo Division Four (waliopata Daraja la Nne) wanakataliwa vyuo vya ualimu,”  alisema.
Alisema, hali ya sasa ni tofauti na miaka ya nyuma kwa kuwa sasa, hata makatibu tarafa wana Shahada.
Kwa mujibu wa tamko la Serikali, kuanzia sasa wanaosomea ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada, sharti wawe na ufaulu wa daraja la tatu.
Aidha, Serikali imeamua kuanzia sasa wanaojiunga na mafunzo ya  Stashahada ya Ualimu katika masomo ya Sayansi wakiwa na ufaulu wa Daraja la Kwanza, watasomeshwa bure. Pia wenye ufaulu wa Daraja la Pili na la Tatu, watapewa mkopo.
Akizungumzia shule za sekondari za kata, Rais Kikwete alipongeza maendeleo ya taaluma, kutokana na baadhi shule hizo  kuwa miongoni mwa wanaofanya vizuri katika mitihani ya taifa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakati shule hizo zinaanzishwa, hali ilikuwa ngumu  tofauti na sasa ambako yapo mabadliko. Alitoa takwimu kwamba kati ya wahitimu 71,000 waliochaguliwa kuendelea na Kidato cha Tano, 20,000 wameachwa.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari, Rais Kikwete aliagiza ifikapo mwaka 2016, kila mwanafunzi awe na kitabu chake.
Alisema, serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili hiyo, zikiwemo Sh  bilioni 21 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2014/2015.
Rais aliagiza fedha kwa ajili ya vitabu zitengwe na azione kwa kuwa anataka taifa lipate wataalamu wengi.
Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema katika shule za msingi hivi sasa, wanafunzi watatu wanatumia kitabu kimoja.
Kwa mujibu wa Mhagama, kupitia  Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Wilaya ya Mbinga ilikuwa ya kwanza kitaifa kwa maendeleo ya elimu.
Aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri, wanayofanya wilayani humo. Alibainisha kuwa walimu 112 waliopangiwa kufundisha katika shule za msingi  walikwenda, na wengine 138 waliotakiwa kwenda kufundisha shule za sekondari, wanaendelea na kazi.

No comments: