IPTL YATAKA MAHAKAMA 'IMFUNGE DOMO' KAFULILA

Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na walalamikaji wengine wawili, wamewasilisha ombi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Walalamikaji hao wanaiomba mahakama hiyo, itoe zuio la muda kwa  Mbunge wa Kigoma  Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kuendelea kutoa kauli za udhalilishaji dhidi yao.
Ombi hilo limewasilishwa siku chache baada ya IPTL na walalamikaji wengine Pan Africa Power Solution (PAP) na Mkurugenzi wa PAP, Harbinger Seth, kufungua kesi ya madai dhidi ya Kafulila, wakimtaka aombe radhi na kuwalipa Sh bilioni 310 kama fidia, kutokana na kutoa kauli za udhalilishaji dhidi yao.
Ombi hilo lilitajwa mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya Jaji Rose Temba na kuahirishwa hadi Agosti 3 mwaka huu.
Katika ombi hilo, lililoungwa mkono na hati ya kiapo ya Seth, walalamikaji hao pia wanaomba Kafulila alipe gharama za uendeshaji wa ombi hilo.
Katika kesi ya msingi, wanamlalamikia Kafulila kuwatuhumu kuchukua fedha kinyume cha sheria katika akaunti ya Escrow iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa madai amewadhalilisha na kuwasababishia hasara kibiashara.
Walalamikaji hayo wanataka Kafulila awalipe Sh bilioni 210 kama fidia ya kutoa kauli za udhalilishaji, kuwasababishia hasara katika biashara na kuharibu mtazamo wa biashara zao.
Aidha, wanaiomba Mahakama iamuru Kafulila, awaombe radhi, pia awalipe Sh bilioni 100 kama hasara ya jumla pamoja na usumbufu walioupata, kutokana na kauli za udhalilishaji.

No comments: