WATU SITA KORTINI KWA ULIPUAJI MABOMU ARUSHA

Watu sita waliokamatwa na polisi juzi, wakituhumiwa kuhusika na ulipuaji wa mabomu katika sehemu mbalimbali jijini Arusha, wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya ugaidi na kufadhili ulipuaji mabomu.
Washitakiwa hao ni Shabani Mussa (27) na  Athumani Mmasi,  ambao wote ni walinzi wa mgahawa wa Vama Traditional Culture ulioko Uzunguni, jijini Arusha.
Wengine ni Mohamed Nuru (38),  Jafari Lema ambaye ni imamu wa Msikiti wa Quba na pia Mwalimu wa Shule ya Msingi Oltunei wilayani Arumeru.
Washitakiwa wengine ni Abdul Mohamed (31) na mfanyabiashara maarufu wa Jiji la Arusha, Said Temba (39).
Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Augustino Kombe alidai mbele ya Hakimu Rose Ngoka,  kuwa mshitakiwa wa kwanza, Mussa na wa pili, Mmasi wanashitakiwa kwa  ugaidi kwa kulipua mabomu katika matukio ya kati ya Februari na Julai mwaka huu.
Alidai miongoni mwa matukio hayo, ni pamoja na la mlipuko katika mgahawa wa Vama Traditional Culture, uliotokana na washitakiwa kurusha bomu la mkono.
Mwendesha mashitaka alidai Mussa anakabiliwa na shitaka lingine la peke yake, ambalo ni la kurusha bomu katika mgahawa na kusababisha watu kujeruhiwa na bomu la mkono alilorusha katika mgahawa huo,  ambao alikuwa mlinzi.
Kombe alidai  shitaka la tatu ni kutoa silaha linalowakabili Mmasi, mshitakiwa nne,  Lema, mshitakiwa wa tano, Mohamed na wa sita, Temba.
Mwanasheria  aliwasomea shitaka la nne, linalowakabili watuhumiwa wote sita la kutoa ushirikiano wa kufanya ugaidi na kutoa fedha kwa watu mbalimbali jijini Arusha, kufanya ugaidi wa ulipuaji mabomu.
Hakimu Ngoka aliwataka washitakiwa wote, kutojibu chochote, kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo. Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka hayo. Kesi hiyo itatajwa tena Agosti 6 mwaka huu.

No comments: