SULUHU BUNGE LA KATIBA KUSAKWA LEO

Wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba, wanakutanishwa leo katika kikao kilichoitishwa na Mwenyekiti, Samuel Sitta.
Kikao hicho kimelenga kutafuta suluhu ya mvutano,uliosababisha baadhi ya wabunge kususa. Kikao hicho cha maridhiano, kitafanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, alikiri kuwepo kikao hicho. Alisisitiza kwamba ni cha wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
“Tumealika wajumbe wote na Kanuni ndizo zinatuelekeza hivyo na hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyetutaarifu ama  kuwa ana udhuru au hauhudhurii, lakini ukweli ni kuwa huu ni mkutano wa kawaida tu,” alisema Hamad.
Kikao hicho kilichoitishwa na Sitta, ikiwemo kutangaza katika vyombo vya habari, lengo ni kukutanisha wabunge wote wakiwemo wanaounda  Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliosusa bunge ili kupata suluhu ya mvutano huo.
Hata hivyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema wabunge wake hawatahudhuria  kikao hicho cha maridhiano kwenye Ofisi ndogo za Bunge.
Hayo yalisemwa na Ofisa Uhusiano wa Chadema, Tumaini Makene alipozungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana.
Makene alisema msimamo wao ni kutohudhuria kikao hicho, kwa madai kwamba anayeuongoza hana uhalali wa kusuluhisha masuala ya Katiba.
“Tayari viongozi wakuu wameshatoa matamko yao, akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa kuwa hawana imani na Sitta kuhusu suala hili, tunazo taarifa za ndani kuwa ametumwa na CCM. Hatuwezi kuhudhuria,” alidai Makene.
Wakati Chadema ikitoa msimamo huo, baadhi ya wabunge wa chama cha NCCR-Mageuzi, ambacho ni mwanachama wa Ukawa, walidai hawana taarifa ya kikao hicho.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alisema hana taarifa kuhusu kikao hicho na kwamba yupo jimboni kwake, akiendelea na shughuli zake za kimaendeleo.
“Siwezi kuzungumzia msimamo wa chama, kwa kuwa sipo makao makuu, niko huku jimboni, sina taarifa wala sijasikia kokote kuhusu kikao hicho,” alisisitiza Machali.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alikiri kusikia taarifa za kuwepo kwa kikao hicho cha leo. Hata hivyo, pia alidai  hajapata mwaliko wowote, unaomtaka kuhudhuria.
“Labda kwa kuwa niko huku kijijini; na unajua sie mialiko yetu inakuja kwa njia ya maandishi, sasa siwezi kuzungumza kwamba tunahudhuria au la, masuala ya Ukawa msemaji wetu ni Mwenyekiti wa chama, James Mbatia,” alisema Kafulila.
Mbatia na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho pia ni mwana Ukawa, walipotafutwa na mwandishi, simu zao zilikuwa zinaita bila majibu.

No comments: