UBORA HAFIFU WAKWAMISHA AJIRA KWA WAHITIMU VYUO VIKUU

Ubora hafifu wa wahitimu wa vyuo vikuu kiasi cha kusababisha wengine kutoajirika, vimeigusa serikali na sasa inatarajia kuja na mpango wa kukabili hali hiyo.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekiri kwamba rejea mbalimbali za waajiri zinaonesha upo  upungufu katika ubora wa wahitimu kiasi cha kutoajirika, jambo ambalo imesema haiwezi kulinyamazia.
“Rejea mbalimbali za waajiri zinaonesha kuna upungufu katika ubora wa wahitimu wa vyuo vikuu na kuwa hawaajiriki,” alisema  Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sylvia Temu.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Temu aliendelea kusema, “...ni jambo ambalo hatuwezi kulinyamazia kama watunga sera,  huwezi kujadili peke yako bali na wadau ili kupata mawazo chanya.”
Serikali katika kuhakikisha suala hilo linapata utatuzi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vishiriki zinatarajia kuja na mpango kuhakikisha vyuo vinatoa wahitimu bora wenye ujuzi wa kuajirika na kujiajiri.
Kaimu Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Magishi Mgasa katika mkutano huo, alisema suala hilo ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa kwa kina kwenye kongamano la elimu ya juu, mjini Arusha.
Mgasa alisema kwa sasa kumekuwapo na mjadala wa kuwepo wahitimu wa elimu ya juu wasio na ujuzi na ambao wamekuwa hawaajiriki na hawawezi kujiajiri.
Kuhusu kongamano, Mgasa alisema litakakwenda sanjari na maonesho ya huduma za vyuo vikuu mbalimbali, yanafanyika kuanzia Agosti 13 hadi 15 chini ya kauli mbiu ‘Elimu ya Juu baada ya Mpango wa Maendeleo wa Milenia baada ya 2015.’
 Mgasa alisema wadau watajadili na kutafakari juu ya maendeleo ya ujuzi kwa kutambua uwezo wa kiuchumi nchini.
“Tutaamua wajibu wa taasisi za elimu ya juu katika kusaidia maendeleo endelevu kupitia maendeleo ya ujuzi katika nchi, tukitilia mkazo aina ya maarifa na ujuzi unaotolewa na taasisi za elimu ya juu na mahitaji halisi ya taifa katika elimu, ujuzi na ushindani,” alisema Mgasa.
Alisema pia kongamano hilo litatambua fursa muhimu ambayo taasisi za elimu ya juu zinaweza kuchagiza wajibu wa maendeleo endelevu ya nchi kwa kulenga kujenga ajira ya wahitimu.
“ Pia tutatumia fursa hiyo kuweka mikakati ya uwezeshaji wa mtandao mkubwa kati ya taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na viwanda na baadhi ya wadau muhimu wa elimu ya juu,” alisema.
Akizungumzia mafanikio ya makongamano yaliyopita,  Temu alisema kupitia jukwaa hilo, wadau wa elimu walikuja na mpango wa miaka mitano (2010-2015) uliolenga kuongeza udahili wa wanafunzi, uwekezaji katika elimu ya juu na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Alisema kupitia mpango huo, Serikali imepunguza tatizo la walimu kwa kusomesha walimu 400 na kati ya hao, wenye Shahada ya Uzamivu ni zaidi ya walimu 120.
 “Nchi ina mabadiliko makubwa, sasa tunazungumza uchumi wa gesi, kuzalisha wataalamu katika sekta za vipaumbele kama utalii, usafiri, hivyo tunataka kushirikiana na sekta binafsi ili kupata fikra chanya,” alisema.

No comments: