MAJINA YA WANAOPIGA MABOMU ARUSHA KUANIKWA HADHARANI

Watuhumiwa wa mabomu katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha, watawekwa hadharani hivi karibuni ikiwa ni pamoja na umma kuelezwa kilichotokea na waliowatuma.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hayo juzi alipokuwa akihutubia sherehe za Baraza la Idd jijini Dar es Salaam.
Alisema ingawa hatua za kisheria zinaendelea kwa baadhi ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi, serikali pia itaweka wazi juu ya matukio hayo ya mabomu, ikiwemo wanaowatuma.
Alisema kinachosubiriwa ni kukamatwa watuhumiwa wengine kama wawili, ambapo aliomba wananchi kushirikiana na Serikali  watiwe mbaroni.
“Serikali haikulala tangu tukio la kurushwa kwa bomu pale  Olasiti, tuliongeza nguvu ya wataalamu wa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na dalili nzuri zimeanza kuonekana.
“Napongeza vyombo vya ulinzi na usalama, tumekamata kundi kubwa na baadhi  yao wamekiri kushiriki mambo kadhaa na tutakuja kuwashirikisha,” alisema Pinda.
Alitaka jamii kufichua watu wote wenye  nia ovu ya uhalifu ili wananchi na jamii nzima iishi kwa amani. Alitaka viongozi wa dini kuepuka mifarakano ndani ya dini kwa kuwa inasababisha chuki zisizo na msingi.
Alisema mifarakano ndani ya dini ni mibaya na inapotoka nje na kuwa kati ya dini moja na dini nyingine, inakuwa mbaya zaidi na kuwasisitizia viongozi wa dini, kuhakikisha kila dini waumini wanakuwa na amani, utulivu na mshikamano.
Pinda alisema  anaamini amani na utulivu wa Tanzania, msingi wake ni mafundisho ya dini. Alisisitiza taifa lolote ambalo halina msingi huo wa dini, watu wake hawana tofauti na wanyama , kwa kuwa hawana hofu ya Mungu na hivyo hawaogopi lolote.
Alipongeza viongozi wa dini wa Dar es Salaam kwa kuunda Kamati ya Amani, inayohusisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo  ambayo hukutana na kujadili  namna ya kuboresha amani bila kujali tofauti zao.
Kutokana na ubunifu huo wa viongozi wa Dar es Salaam,  Pinda alisema kila mkoa anaokwenda, amekuwa akiwahamasisha wakuu wa mikoa kusaidia kuandaa kamati kama hizo kwa kuwa ni msingi wa amani.
Baraza la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) wilayani   Arumeru,  limeahidi  kushirikiana na  polisi mkoani kuhakikisha linafichua watu ambao wamekuwa wakijihusisha na uvunjifu wa amani mkoani Arusha.
Kiongozi wa Baraza la Wazee, Wilaya ya Arumeru, Shehe Haruna Husein  alisema hayo jana akizungumza na waandishi wa habari kulaani vikali vitendo mbalimbali vya uhalifu vinavyoendelea mkoani humo.
Alisema, “Bakwata wilayani Arumeru inalaani vikali vitendo hivyo vya uhalifu vinavyoendelea mkoani hapa.” Alisisitiza watashirikiana na polisi kufichua wahilifu.
Alipongeza Polisi kwa jitihada zao kudhibiti uhalifu. Alitoa mwito kwa wahisani wengine kuhakikisha wanashirikiana na jeshi hilo kuwezesha wahalifu wakamatwe.
“Kwa kweli sisi kama Bakwata tunalaani vikali sana hivi vitendo vya uhalifu vinavyoendelea mkoani hapa, huku tukiahidi kushirikiana na jeshi la polisi katika kudhibiti matukio ya uhalifu yanayoendelea mkoani hapa ili wahalifu wote wanaojihusisha na matukio hayo wachukuliwe hatua kali za kisheria,” alisema.
Miongoni mwa matukio ya ulipuaji mabomu ni pamoja na kwenye Kanisa Katoliki, Parokia ya Joseph Mfanyakazi, Olasiti. Katika tukio hilo, watu wawili walipoteza maisha na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Tukio lingine la ulipuaji bomu, ni kwenye mkutano wa wa Kampeni za uchaguzi mdogo wa Madiwani wa Chadema katika eneo la Soweto, ambalo pia watu kadhaa walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Hivi karibuni, mlipuko mwingine ulitokea katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine na kusababisha majeruhi. Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika katika ulipuaji wameshafikishwa mahakamani.
Tukio lingine la hivi karibuni ni la Katibu wa Bakwata, mkoani Arusha, AbdulKarim Jonjo aliyejeruhiwa na mgeni wake baada ya kurushiwa bomu nyumbani kwake, eneo la Esso wakati akipata daku na mgeni wake.

No comments: