TANZANITE YA SIHILINGI BILIONI 10 ILIYOIBWA YAFICHWA SAKINA

Madini ya tanzanite kilo 15 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 10 ya kampuni ya Tanzanite One yaliyoibwa hivi karibuni wilayani Simanjiro katika Mkoa wa  Manyara,  yanadaiwa kufichwa eneo la Sakina na baadhi ya wauzaji wakubwa wa madini hayo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit  Nsimeki alisema wamepata taarifa hizo na kwa sasa watu saba wanashikiliwa. Alisema hawawezi kutaja majina yao, kwa sababu za kiupelelezi.
Kwa mujibu wa kamanda, simu za watuhumiwa zimechukuliwa na polisi na wanafanyia kazi mawasiliano ambayo yamewezesha kugundua baadhi ya mambo muhimu.
"Taarifa za awali zinadai madini yaliyoibwa yako Sakina Arusha kwa wafanyabiashara wakubwa na vigogo wa biashara hiyo, lakini na sisi tunafuatilia taarifa hiyo na nyingine nyingi na simu za watuhumiwa wa awali tunazishikilia kwa sasa,’’alisema.
Wakati huo huo, Shirika la Madini la Taifa (Stamico)  limekanusha taarifa zinazohusisha wafanyakazi wake katika kupanga mipango ya wizi wa madini hayo.
“Tunapenda kuutaarifu umma wa Watanzania kuwa taarifa hiyo si ya kweli na kwamba haina takwimu sahihi kwa mujibu wa wahusika wa pande zote mbili waliotajwa katika habari hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa ya Stamico ikikariri gazeti moja la kila siku lililoandika habari hizo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makadirio ya thamani ya madini yaliyoibwa kutoka Main Shaft siku hiyo Julai 17 mwaka huu ni kilo 15, zinazokadiriwa kuwa na thamani ya dola za Kimarekani  47,105.01 .
Shirika hilo limesema kulingana na taarifa lilizo nazo, kulikuwa na mfuko wa kilo 23 za madini hayo uliokutwa katika gari lililohusika katika wizi huo.
Stamico imesema inasubiri namna polisi, itakavyowasaidia kuwapata wezi na madini yaliyoibwa, mkondo wa sheria uchukue nafasi yake dhidi ya wezi walioiingizia serikali hasara kubwa.
Mgodi wa Tanzanite wa Mirerani, unamilikiwa kwa pamoja kati ya Stamico na kampuni ya Tanzanite One Ltd kwa asilimia 50 kwa kila upande.

No comments: