BEI YA MAFUTA SASA KUSHUKA

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza mchakato wa kutafuta namna ya kupunguza gharama za uingizaji wa mafuta nchini.
Hatua hiyo itawezesha pia bei ya nishati hiyo  nchini kushuka.
Chini ya mchakato huo, Ewura inataka kushusha gharama za uagizaji wa mafuta, kwa kuchagiza  ushindani wa upatikanaji wa mitaji ya fedha za uagizaji nishati hiyo.
Inataka katika ushindanishaji wa watoaji wa fedha ambao ni benki, hatimaye kuwe na ulinganifu wa upatikanaji fedha hizo miongoni mwa kampuni za mafuta.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema jijini Dar es Salaam jana, baada ya kufanikiwa katika utaratibu wa uingizaji mafuta wa pamoja, sasa wameamua kukutana na wadau kujadili namna ya kushusha zaidi gharama za nishati hiyo muhimu.
Mkutano huo wa wadau ulikutanisha washiriki mbalimbali, ikiwemo Benki Kuu (BoT), kampuni za mafuta, benki za biashara.
Ngamlagosi alisema uingizaji  wa pamoja wa mafuta, umesaidia kuokoa muda na gharama kubwa za fedha zilizokuwa zikilipwa kutokana na meli
kukaa muda mrefu.
Mjadala huo umelenga mambo mawili makuu, yatakayowezesha kushuka kwa nishati hiyo.
Mkurugenzi huyo mkuu wa Ewura alisema kwanza wanaangalia namna ya kuweka ushindani wa benki katika ulipaji wa huduma za mikopo ya kampuni, ambazo zinaingia mkataba kwa ajili ya ununuzi wa mafuta.
"Kwa mfano, kwa sasa ni asilimia moja ambayo inalipwa na mlaji, lakini bado tunataka tuangalie iweze kushuka zaidi ya hapa. Kwa mfano nchi ya Msumbiji,  kampuni zinalipa kati ya asilimia 0.3 mpaka 0.4 kwa hiyo na sisi
tufike huko," alisema Ngamlagosi.
Alisema jambo lingine ni kurekebisha barua za benki kwa ajili ya kuruhusu upakuaji wa mafuta. Alisema katika uagizaji wa pamoja wa mafuta, meli moja inakuwa na mafuta ya kampuni nne au tano na ikitokea mmoja akashindwa kuwasilisha barua husika, hukwamisha ushushaji wa mafuta.
“Hapa ikitokea mmoja akashindwa kuleta 'letter of credit' (barua) kutokana na kushindwa kuelewana na benki, anakwamisha mzigo wa watu wote, kwa hiyo hata hii tutaangalia namna ya kurekebisha," alisema.
Kwa mujibu wake, kwa sasa suala hili wamelileta kwa ajili ya majadiliano na kupata mawazo ya wadau wa sekta hiyo.
Mpango huo utakapofanikiwa, utatoa unafuu kwa mtumiaji wa mwisho ambaye ni mlaji.
Aidha,  utaratibu wa uingizaji wa mafuta kwa pamoja umebainika  kupunguza gharama kubwa na hivyo kuwa nafuu kwa walaji na uchumi wa nchi. Taarifa ya mamlaka inasema utaratibu huo umeokoa takribani Sh bilioni 126 ambazo hutumika.
"Hata gharama zimepungua sana. Zamani meli moja ilikuwa inakaa karibu siku 40 hadi 60 na kwa siku zinakaa meli tano mpaka sita, ambazo zote ilikuwa
lazima uzilipie dola za Marekani 20,000 kwa hiyo ilikuwa gharama kubwa sana," alisema.
Alisema manufaa hayo yaligunduliwa baada ya utafiti ulioafanywa na  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Uchumi.
Alisisitiza kwamba utaratibu huo umekuwa na manufaa. Alisema ni muhimu kuangalia njia nyingine za kushusha gharama zaidi.
Mmoja wa wadau aliyehudhuria mkutano huo kutoka Kampuni ya Petroleum Importation Co-ordinator Ltd,  Raymond Lusekelo, alisema mipango hiyo
ya kushusha gharama zaidi ni mizuri, ikiwa itatekelezwa ipasavyo.
Lusekelo, ambaye ni Meneja Mipango wa kampuni hiyo, alisema anaamini hata wafanyabiashara wengine wa nishati hiyo, hawana tatizo na mpango huo, ambao unaonekana utaleta nafuu zaidi kwa watumiaji wa mwisho wa  mafuta.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura alisema Agosti 4 mwaka huu,  itakuwa mwisho wa kupokea maoni kutoka kwa wadau,  kueleza ni kwa namna gharama zishuke.
Baada ya kufunga mchakato wa kupokea maoni, watapanga tena siku ya kukutana na wadau wa karibu hususani kampuni za mafuta. Baada ya hapo, Ewura itaeleza mapendekezo juu ya maoni yaliyokusanywa.

No comments: