SERIKALI YAVUKA LENGO USAMBAZAJI UMEME

Serikali imekiomba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuipangia upya malengo ya kusambaza umeme kwa wananchi kwa sababu malengo yaliyopangwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 yamefikiwa na kupitwa hata kabla ya kumalizika kipindi cha miaka mitano.
Aidha, Serikali imesema kuwa upo uwezekano mkubwa kwamba usambazaji wa umeme unaweza kufikia asilimia 50 ya wananchi wote wa Tanzania ifikapo mwakani kwa sababu umeme sasa unasambazwa kwa kasi isiyokuwa ya kawaida.
Ombi hilo la Serikali lilitolewa juzi na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, wakati alipozungumza katika mkutano wa hadhara ambao umehutubiwa na Rais Jakaya Kikwete, mjini Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Waziri Muhongo ameuambia umati huo wa wananchi kuwa Ilani ya uchaguzi ya CCM ilikuwa imeipa Serikali jukumu la kusambaza umeme kufikia asilimia 30 ya wananchi.
"Hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Rais tayari tumevuka lengo hilo na kufikia asilimia 36 na kwa kasi hii tunayokwenda nayo haitashangaza kama tufikia asilimia 40 ama hata 50 ya kuwasambazia wananchi umeme."
Ameongeza Waziri Muhongo: "Hivyo, tunakiomba chama chetu kitupangie malengo mapya yanayokwenda na kasi mpya ambayo Wizara yangu inaionyesha. Tunataka chama kitupe malengo mapya kwa sababu yale tuliyopewa tumevuka, tena kwa mbali."
Kuhusu usambazaji wa umeme katika Wilaya ya Nyasa, Waziri Muhongo amesema vijiji 58 kati ya vijiji 73 vya wilaya hiyo vitasambaziwa umeme katika mradi ambao tayari umeanza ikiwa ni idadi ya juu ya usambazaji umeme vijijini. Mradi huo uliozinduliwa jana na Rais Kikwete mjini Mbamba Bay unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.
Kuhusu hali ya umeme ilivyo mkoani Ruvuma, Muhongo alisema kiasi cha Sh bilioni 26.5 kimetengwa kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kusambaza umeme mkoani humo. Hata hivyo, alisema mkoa huo una uwezo wa kutosha wa kuzalisha umeme wake wenyewe.

No comments: