NMB YAIPIGA JEKI VIFAA HOSPITALI YA SINZA

Hospitali ya Sinza jijini hapa inakabiliwa changamoto kadhaa, ikiwamo upungufu wa vifaa tiba na vitanda katika wodi ya wazazi.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa vifaa kutoka Benki ya NMB, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Benedict Luoga alisema pamoja na juhudi za serikali kuihudumia hospitali hiyo bado ina upungufu huo.
Alisema uwezo wa hospitali ni kupokea wastani wa wagonjwa 32 kwa ajili ya kujifungua, lakini wamekuwa wakifikia wajawazito 70.
“Uwezo wa hospitali ni kupokea wagonjwa 32, ukifika msimu wa kujifungua Januari hadi Mei hufikia wajawazito zaidi ya 70 kwa wakati mmoja, jambo ambalo linatupa ugumu katika kutoa huduma,” alisema Dk Luoga.
Akizungumzia msaada wa vitanda na vifaa mbalimbali vya kujifungulia vyenye thamani Sh milioni 10 kutoka NMB, Luoga alisema msaada huo utaongeza ufanisi hospitalini hapo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja NMB kanda ya Dar es Salaam, Salie Mlay alisema mwaka huu benki yake imetenga zaidi ya Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi ikiwamo kusaidia sekta ya afya na elimu.
Walionufaika mbali ya hospitali ya Sinza ni Same, Kilimanjaro waliopewa vifaa vya kujifungulia vikiwamo vitanda na magodoro vya thamani ya Sh milioni 15, kituo cha afya cha Buzuruga, Mwanza Sh milioni 4.4.

No comments: