'MVUA ZINAZONYESHA NI MABADILIKO YA HALI YA HEWA'

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua zilizonyesha kuanzia alfajiri ya jana zinatokana na mabadiliko ya hali ya hewa baharini na zinatarajia kuendelea leo katika maeneo yote ya pwani.
Imesema hali hiyo pia imesababisha kuwepo kwa upepo mkali na mawimbi katika Pwani ya Kusini hivyo kuwatahadharisha wananchi wa maeneo hayo kutotumia vyombo vya baharini.
Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dk Agness Kijazi alisema kwa sasa hakuna msimu wa mvua hivyo mvua hizo ni za kawaida kutokana na kuwepo kwa mgandamizo mdogo wa hewa baharini na kusababisha mvua kwa baadhi ya maeneo.
Alisema ingawa mvua hizo ni za kawaida lakini pia kutakuwa na  upepo mkali wa kilometa 40 kwa saa na mawimbi yenye ukubwa wa mita mbili katika maeneo ya Pwani ya Kusini.
“Tutaendelea kutoa tahadhari lakini hali hiyo itadumu kwa  usiku wa leo mpaka kesho (leo), hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua hatua stahili hasa kwa wale wanaotumia vyombo vya baharini,” alisema Dk Kijazi.
Dk Kijazi alisema mabadiliko hayo yatasababisha mvua kidogo katika maeneo yote ya Pwani  mpaka Mkoa wa Mtwara  huku upepo na mawimbi ukiathiri mikoa ya Lindi na Mtwara.

No comments: