MTANDAO WA TAASISI ZA WAKURUGENZI AFRIKA WAPANUKA

Mtandao wa Taasisi za Wakurugenzi Afrika (ACGN) umezidi kukua kwa kupata wajumbe wapya wawili katika mkutano wake jijini Dar es Salaam.
Wajumbe waliosaini makubaliano na mtandao huo ni Taasisi ya Wakurugenzi kutoka Tunisia na Kituo cha Utawala Bora cha Misri.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika mkutano wa mtandao huo uliomalizika jijini hivi karibuni.
Kituo cha Utawala Bora wa Mashirika Taasisi ya Wakurugenzi Ethiopia nayo iko katika mchakato wa kujiunga na ilihudhuria mkutano huo kama mtazamaji tu.
Pia mtandao huo ulifikia makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Maadili ya Afrika ya Kusini pamoja na Taasisi ya Kimataifa ya Uhasibu, ACCA.
“Tunazidi kukua lakini bado kazi ni kubwa...tunahitaji wanachama wengine zaidi,” alisema Ofisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa ACGN, Said Kambi.
Mtandao huo kwa sasa  una wanachama ambao ni taasisi kutoka nchi 13 na washirika wengine saba huku Kambi akisema ushirikiano na Taasisi ya Maadili ya Afrika ya Kusini utasaidia kuimarisha maadili katika uendeshaji wa mashirika Afrika wakati ushirika na ACCA utasaidia kutoa mafunzo ya kitaalamu, utafiti na kubadilishana taarifa.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wakurugenzi Kenya, Meshack Jerome alisema utawala bora wa mashirika ni kitu muhimu kwa maendeleo ya nchi za Afrika ya Mashariki.
Alitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuhakikisha zinazingatia uongozi bora wa mashirika ili kufikia maendeleo endelevu.
“Taasisi hii iliyoanza mwaka 2004 imesaidia kwa kiwango kikubwa nchi yetu kupambana na ufisadi na kuimarisha maadili katika nchi yetu,” alisema.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Maadili Afrika ya Kusini, Profesa Deon Rossouw alisema utawala bora wa mashirika unahusu kuendesha mashirika kwa mafanikio na kwa uwazi.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa ACGN,  Jane Valls alishauri serikali za Afrika  kufikiria kuwa na mwongozo thabiti utakaoweka viwango, na maadili yatakayopaswa kufuatwa na mashirika.
Valls ambaye pia ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wakurugenzi Mauritius (MIoD) alisema uendeshaji wa mashirika na kampuni ni jambo la muhimu kwa maendeleo endelevu ya nchi yoyote.
Alisema kuwa uendeshaji bora wa mashirika barani Afrika ni muhimu kwa sasa ambapo biashara miongoni mwa mataifa ya Afrika inakuwa  pia na  mitaji ya uwekezaji barani humo inazidi kuongezeka.
Waanzilishi wa mtandao huo walikuwa ni Taasisi za Wakurugenzi kutoka Kenya, Malawi, Mauritius, Morocco, Msumbiji, Afrika ya Kusini na Tanzania. Wengine ni taasisi za Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Mtandao huu unalenga kujenga uwezo wa taasisi wanachama na kuendeleza uendeshaji bora wa mashirika katika sekta binafsi na umma barani Afrika.
 ACGN iliundwa kujenga uwezo wa wanachama wake kuimarisha uendeshaji wa mashirika, na kujenga mashirika bora barani Afrika miongoni mwa mambo mengine.
Mtandao huo pia unatoa fursa kwa watunga sera na wadau wengine kujadiliana kuhusu masuala  mbalimbali yanayohusu changamoto mbalimbali  na uendeshaji wa mashirika na kampuni barani Afrika.

No comments: