WASIFU USHIRIKIANO WA MZUMBE, CHUO KIKUU AFRIKA KUSINI

Serikali na sekta binafsi nchini zimesifu ushirikiano wa kitaaluma uliozinduliwa kati ya vyuo vikuu vya Mzumbe na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Stellenbosch cha Afrika ya Kusini.
Taasisi hizo zimeingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya Menejimenti kwa maofisa wa Serikali na sekta binafsi nchini na Afrika ya Mashariki kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema ushirikiano huo ni hatua nyingine ya maendeleo kwa taifa.
Naibu Waziri huyo aliyewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Adolph Mkenda alisema Serikali inakaribisha ushirikiano huo ambao alisema unaendana na mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa.
“Watanzania watafaidika na mpango huu ambao masomo yake yatakuwa yanatayarishwa na wataalamu kutoka vyuo hivi viwili,” alisema na kuongeza kuwa Serikali ingependa kuona ushirikiano kama huu zaidi nchini.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni, Dk Elisante Gabriel alisema ushirikiano huo umekuja wakati mwafaka.
“Nawatakia mafanikio na nashauri kampuni hapa nchini kupeleka maofisa wake kusoma programu hizo zitakazokuwa zinatolewa Mzumbe,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisifu uhusiano huo na kusema wadau wa sekta wanahitaji mafunzo kama hayo.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa Kitengo kinachotoa mafunzo hayo katika Chuo Kikuu cha Stellenbosch, Profesa Frik Landman alisema kama sekta binafsi na Serikali wataona umuhimu, uhusiano huo utakuwa chachu ya maendeleo ya Tanzania na Afrika Kusini.
Alisema ni muhimu na ni jambo la thamani kwa taasisi katika nchi zikawa na mameneja wenye ufanisi kuzalisha na kuleta tofauti.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Fedha na Utawala, Profesa Faustin Kamuzora alisema uhusiano huo unatokana na mpango mkakati wa chuo hicho unaolenga kushirikiana na taasisi toka sekta za umma na binafsi.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Mafunzo hayo hapa nchini, Profesa Shiv Tripathi awamu ya kwanza ya mafunzo hayo itatolewa jijini katika chuo hicho kwa siku mbili.

No comments: