MTAALAMU AONYA KUHUSU NYAMA MBICHI, MAZIWA

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi imewatahadharisha wananchi hasa wa jamii za wafugaji kuacha mazoea ya kunywa maziwa yasiyochemshwa pamoja na kula nyama mbichi ili kujiepusha na hatari ya kuambukizwa magonjwa ya mifugo.
Imesema ulaji wa vyakula hivYo ikiwemo damu mbichi ya wanyama kama ng’ombe na mbuzi, huchochea maambukizi ya ugonjwa hatari wa kutupa mimba
(Brucellosis) unaoishambulia mifugo ambao kwa binadamu usiposhughulikiwa mapema husababisha
kifo.
Hadhari hiyo ilitolewa na timu ya madaktari wa mifugo kutoka wizarani waliotembelea wilayani Korogwe hivi karibuni kwa lengo la kushughulikia matatizo ya mifugo.
Wataalamu hao walitembelea vijiji vya Kweisewa kata ya Mkalamo na Changalikwa kilichopo kata ya Magamba -Kwalukonge ,ambavyo vimeathiriwa na ugonjwa wa kutupa mimba ambapo hivi sasa unadaiwa umeanza kuathiri afya za wafugaji.
Mmoja wa madaktari hao, Henry Magwisha alisema tayari ugonjwa huo umeenea kwa baadhi ya wananchi ambao wameonesha dalili za kuumwa kichwa, kutoka
jasho, kupoteza uzito, homa za vipindi na pamoja na maumivu ya mwili kwa ujumla.
“Idadi kubwa ya binadamu wanaoambukizwa vimelea vya ugonjwa huu wa brucellosis hudhani kwamba wanaugua malaria kama baadhi yenu mlivyo sasa…ila wengine wanapata kuumwa na tumbo wakihisi kuwa ni typhoid…lakini utofauti unakuja hapa kwamba binadamu mgonjwa mwenye vimelea hivi anaweza kurejea matibabu
ya ugonjwa anaohisi mara kadhaa pasipo kupona kama ilivyo kawaida”, alisema.
Alitaja dalili za ugonjwa huo kwa wanyama ni kutupa mimba kipindi cha miezi mitatu ya mwisho, wengine kuzaa ndama mdhaifu au aliyekufa, mnyama kuzaa na kubakiza kondo la nyuma na kwa upande wa dume huvimba kende.
Akizungumzia namna ambavyo maambukizi yanaweza kumpata mfugaji, Magwisha alisema hutokea wakati anapojaribu kumsaidia mnyama anayezaa bila kuvaa glovu mikononi, kutoa ndama aliyekufa, kushika majimaji ya uzazi au kondo la nyuma la mnyama, kunywa damu na maziwa mabichi ya mnyama mgonjwa na hata kula nyama mbichi.
Naye daktari wa Zahanati ya Rosmini inayomilikiwa na kanisa Katoliki kwenye kijiji cha Magamba Kwalukonge, Emmanuel Joseph alisema baada ya kuwafanyia vipimo baadhi ya wananchi amebaini kuna idadi kubwa ya wagonjwa kutoka jamii ya wafugaji kwamba wameambukizwa vimelea hivyo bila kujua.

No comments: