MRITHI WA ASKOFU LAIZER KKKT KUJULIKANA LEO

Hatima ya kinyang’anyiro cha kumpata mrithi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Thomas Laizer aliyefariki mapema mwaka huu, inajulikana leo.
Mkutano wa wajumbe zaidi ya 300 wa Mkutano Mkuu wa 23 wa dayosisi hiyo, unafanyika jijini hapa na  Mkuu wa KKKT nchini, Dk Alex Malasusa  atatoa neno kuu na kusimamia uchaguzi wa kumpata askofu wa kanisa hilo. 
Askofu Dk Laizer alifariki dunia Februari 6 mwaka jana katika Hospitali ya Rufaa ya Selian jijini hapa kutokana na shinikizo la damu.
Akizungumza na mwandishi ofisini kwake, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati,  Samuel Ole Saiguran,  Katibu wa Misheni na Uinjilisti wa dayosisi hiyo, Mchungaji Philemoni Mollel  alisema  wajumbe wa Halmashauri Kuu ya dayosisi hiyo walikutana  kupokea majina ya wagombea wa nafasi  hiyo.
Majina hayo ni kutoka katika majimbo matano ya Dayosisi hiyo ambayo ni Arusha Mashariki, Arusha Kusini, Maasai Kaskazini, Maasai Kusini na Babati.
Licha ya maaskofu wa KKKT, wengine watakaohudhuria ni Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu na Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro, Stanley Hotay.

No comments: