BARUTI YAUA WAWILI NA KUJERUHI WATATU MIRERANI

Wachimbaji wadogo wawili wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamekufa na wengine watatu wamejeruhiwa baada ya kupigwa na baruti wakiwa mgodini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki alisema tukio hilo ni la  juzi saa 7:30 mchana, eneo la Kitalu B Mirerani katika mgodi wa Mike Oscar (34), mkazi wa Sanya Juu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Nsimeki alisema chanzo cha tukio hilo ni mgodi unaomilikiwa na Valerian Palangyo kulipua baruti chini mgodini na kusababisha vifo hivyo vya watu wawili na majeruhi watatu kwenye mgodi wa jirani yao.
“Wachimbaji wa migodi hiyo miwili walikuwa wanaendelea na kazi migodini mwao na baruti ilipigwa kwenye mgodi wa Palangyo ilitoboa  na mgodi wa Oscar na kusababisha mauaji hayo na kujeruhi wengine,” alisema.
Alitaja waliokufa ni Bernad Fredrick (28) na Kuii Habi (32), wote wakazi wa mji mdogo wa Mirerani. Miili yao imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.
Kamanda alitaja majeruhi  ni Adam Juma (29) aliyeumia kifua na mgongo na Hussein Emili (32) aliyepata mshituko, wote wakazi wa Mirerani.
Majeruhi mwingine ni  Reuben (32), mkazi wa Karangai wilayani Arumeru, aliyeumia sikio na shavu la kulia. Polisi wanaendelea kuchunguza tukio hilo.

No comments: