MAWAKILI KWENDA MAREKANI KUSOMEA SHERIA ZA MAFUTA, GESI

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wakishirikiana na The Colom Foundation INC na Nashera Hotel wanakusudia kuwapeleka mawakili 20 wa Tanzania katika Chuo Kikuu cha Mississippi nchini Marekani kujifunza zaidi juu ya elimu ya nadharia na vitendo katika sheria, hususan ya gesi na mafuta.
Hayo yalisemwa jana na makamu wa rais wa chama cha wanasheria Tanganyika, Flaviana Charles wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema chama hicho pamoja na majukumu mengine, kina jukumu la kusimamia upatikanaji wa elimu ya sheria hivyo ushirikiano huo wa kuwapatia mawakili mafunzo ni njia mojawapo ya kuboresha, kusimamia na kuwaongezea mawakili ujuzi na uwezo wa kulinda haki na usawa katika jamii.
Alisema mafunzo hayo yatakuwa ni ya miezi mitano yatakayoanza Septemba mosi mwaka huu na kutarajiwa kumalizika Januari mwakani na watasoma masomo matatu ambapo somo mojawapo la lazima kusoma ni somo la mafuta, na gesi na madini.
Rais wa The Colom Foundation INC na Nashera Hotel, Wilbur Colom ambaye ni mwekezaji hapa nchini, alisema  mafunzo hayo hadi kumalizika yatagharimu kiasi cha dola 12,500 (Sh milioni 20.3) kwa kila mwanafunzi, hivyo wao kama wawekezaji watahusika moja kwa moja katika kuleta maendeleo katika nchi waliyowekeza na kuwa wanajiona ni sehemu ya Taifa.

No comments: