MAASKOFU WANAWAKE TANZANIA 'BADO KWANZA'

Pamoja na majimbo mawili ya kanisa la Anglikana nchini kuruhusu wachungaji wanawake, uamuzi wa kuwapa au kutowapa Uaskofu wanawake unategemea makubaliano ya mkutano wa Sinodi ya Anglikana nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Dk Dickson Chilongani  wakati alipoulizwa na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusu kama lipo tamko lolote kuhusu maamuzi ya Kanisa la Anglikana Uingereza la kutoa daraja la Uaskofu kwa wanawake.
Alisema kanisa la Anglikana nchini linabaki na utamaduni wake hadi hapo Sinodi itakapoketi na kuona kama ipo sababu ya kubadili desturi iliyopo.
Hata hivyo, amesema hakuna kikao cha Sinodi kilichoitishwa kujadili maamuzi ya kanisa la Uingereza na athari yake kwa kanisa la Tanzania. Makao makuu ya kanisa la Anglikana yapo Uingereza.
Katibu huyo alisema maamuzi ya Kanisa la Uingereza hayana uhusiano na kanisa la Tanzania kutokana na ukweli kuwa mfumo wa maamuzi wa kanisa la Anglikana iko tofauti na Wakatoliki, wao upo kwa majimbo husika.
Alisema kwa utaratibu kila jimbo katika kanisa hilo linajitegemea na kwamba uamuzi wa kanisa la Uingereza la kuruhusu kuwapo kwa maaskofu wanawake hakuna uhusiano na msimamo wa kanisa la Tanzania.
Hivi karibuni Baraza Kuu la kanisa la Kianglikana Uingereza, (The General Synod), liliidhinisha wanawake kuwa maaskofu. Uamuzi huo wa kutoa daraja la uaskofu kwa wanawake kunafanya kanisa hilo la Uingereza kuungana na majimbo mengine 20 ambayo yanatoa daraja la uaskofu kwa wanawake.
Majimbo hayo yapo katika nchi za New Zealand, Australia, Marekani, Canada na Afrika Kusini.
“Sinodi ya Tanzania bado hatujadili suala la wanawake kuwa maaskofu mpaka hapo tutakapojadili, msimamo wetu hauwezi kulazimishwa na msimamo wa kanisa la Uingereza,” alisema Dk Chilongani.
Majimbo ya Tanzania ambayo yana wachungaji wa kike ni Dayosisi ya Central Tanganyika Dodoma na Mara.
“Pamoja na majimbo hayo kuwa na wachungaji wa kike, wachungaji hawa hawawezi kuwa maaskofu kwa kuwa maamuzi ya kisinodi hayajafikiwa,” alisema Dk Chilongani.
Hivi karibuni Kasisi Moses Bushendich kutoka kanisa la Kianglikana Uganda akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza ( BBC) alisema kuwa kanisa la Afrika limegawanyika juu ya maaskofu wanawake kutokana na mafundisho ya Biblia.
''Kanisa la Afrika halina uamuzi wa pamoja juu ya suala hili. Kila tawi limechukua msimamo wake baadhi wanapinga na wengine wanaunga mkono,'' amesema Kasisi Bushendich.

No comments: