BENKI YA UCHUMI YAZIDI KUCHANJA MBUGA

Benki ya Uchumi (UCB) iliyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, imetangaza faida ya Sh milioni 599.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14, ikilinganishwa na faida ya Sh milioni 524.2 kwa mwaka jana.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa wanahisa uliofanyika ukumbi wa Hosteli za Uhuru mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Uchumi, Wilson Ndesanjo, alisema faida ya taasisi hiyo imetokana na kutanua wigo na kuimarisha mtandao wa wateja.
Alisema mbali na faida hiyo, pia ongezeko la thamani kwa mwanahisa limefikia asilimia 16.25, ikiwa ni ongezeko la juu la lengo lililowekwa katika mpango mkakati wa kufikia asilimia 14.
Alisema benki hiyo katika kufanikisha malengo yake imejipanga kuongeza mtaji kutoka Sh biloni 2.5 hadi kufikia Sh bilioni 7 ifikapo mwaka 2017, ili kuimarisha ukwasi, utoaji mikopo,  kupanua huduma na kukidhi sheria za Benki kuu (BoT).

No comments: