SHULE ZA GREEN ACRES ZADAIWA KUTIRIRISHA MAJITAKA

Shule za Msingi na Sekondari za Green Acres zilizopo Tegeta Salasala, jijini Dar es Salaam, zinadaiwa kutiririsha maji ya kinyesi kupitia mkondo wa maji ya mvua.
Imeelezwa kuwa tabia hiyo inaathiri makazi ya wananchi waishio eneo jirani na shule hizo.
Mkondo huo wa maji ya mvua, ulichimbwa wananchi wa Salasala, kwa lengo la kuondoa adha ya maji ya mvua na mazalia ya mbu.
Akizungumza na gazeti hili juzi jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Wazo, Atilio Maginga alisema kufuatia tatizo hilo, waliuandikia uongozi wa shule hizo barua na kutoa agizo la siku 14, kuacha kutiririsha maji machafu ya kinyesi, kwani mtaro huo haukuchimbwa kwa ajili hiyo.
 “Nilishatembelea eneo hilo mara mbili, na kukuta maji hayo yakitiririka katika chemchemi, kama hatambui kuwa kuna wakazi wanatumia maji hayo,”alisema Maginga.
Alisema muda waliopewa wa siku 14, haujaisha na kwamba wataendelea kufuatilia suala hilo na kuchukua hatua zaidi, ili kuhakikisha uharibifu huo wa mazingira unasitishwa.
Ofisa Afya wa kata hiyo ambaye alizungumza kwa masharti ya kutotaja jina, alisema walitembelea shule hizo kupulizia dawa ya ugonjwa wa Dengue na kukuta chemba za maji taka zimejaa na kutiririka katika makazi ya watu na kutoa maelekezo kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, Mjumbe wa mtaa wa Salasala, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mussa alisema Uongozi wa Serikali ya Mtaa ulimuandikia barua Mkurugenzi wa shule hiyo na kwamba hakuna hatua alizochukua.
 Alisema tatizo hilo ni la muda mrefu na wananchi wa maeneo hayo wanaendelea kuteseka na harufu ya kinyesi na pia wanahofia usalama wa watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shule hiyo, Edger Rushaigo alisema tatizo lililopo ni kwamba ujenzi wa mabomba ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) katika maeneo hayo, yamechangia kuzuia maji ya mvua ambayo yalikuwa yakitoka katika mto Salasala ambao umepita katika shule yao na kusababisha maji hayo kukwama.
Aliongeza kuwa wasingekubali kuona maji taka yanatiririka wakati kuna wanafunzi wa bweni ambao wanaishi shuleni hapo hivyo wangehatarisha afya zao.
Hata hivyo, Rushaigo alikataa kuwapeleka waandishi wa habari katika maeneo ya ndani ya shule hizo na kudai kuwa tatizo lipo nje ya shule.
Naye mkazi wa maeneo hayo, maarufu kama mama Jack alisema maji hayo hayaambatani na maji ya mvua na kwamba chemba walizozijenga zimebomoka na kuruhusu maji taka kupita katika makazi ya watu.
Alisema Dawasa iliwaita waathirika wa maeneo hayo, Mkurugenzi wa shule hiyo, na wafugaji wa kuku kiwanda cha Interchick na kuambiwa kuwa waondoe maji hayo kwani mabomba yanayopita ni ya maji safi.
‘’Majirani wote tulikutana kutafuta suluhisho kwa kuwasaidia kuondoa maji hayo, lakini hawakutuelewa, Dawasa pia waliingilia kati na kuwapa saa tano za kuondoa maji yaliyokuwa yametuama, lakini kama hawasikii,’’alisema Mama Jack.
Aliongeza kuwa walijenga kwa makusudi chemba hizo katika mkondo wa maji ili wapate kisingizio kwamba maji hayo ni ya mvua jambo ambalo si kweli.

No comments: