ASASI ZATAKA UCHAGUZI WA MITAA UWE MWAKANI

Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Shirika la Policy Forum, linalowakilisha zaidi ya asasi 70 za kiraia kimependekeza uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ufanyike mwakani pamoja na Uchaguzi Mkuu Oktoba.
Mwenyekiti wa Kikundi Kazi hicho, Hebron Mwakagenda alisema lengo ni  kupunguza gharama, kutoa nafasi ya kubadilisha sheria za uchaguzi na kufanya maandalizi mengine ili kuwa na uchaguzi huru na wenye ufanisi mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam juzi, alisema sasa nchi iko katika mchakato wa Katiba mpya, uandikishaji katika daftari la wapigakura na uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa.
 “Tunaungana na Rais Jakaya Kikwete kuwa Tanzania kama nchi sasa iko kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya, hivyo haiwezi kuhimili mchakato wa Katiba na chaguzi mbili kuu…hivyo tunapendekeza uchaguzi wa Serikali za Mitaa ufanyike pamoja na Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015,” alisema.
Alitoa mfano wa Kenya na Zimbabwe, ambazo zimefanikiwa kuunganisha uchaguzi zote mbili.
Alisema uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ulitakiwa kufanyika kati ya Septemba na Oktoba 2014, lakini kumekuwa na matamshi mbalimbali ya viongozi, hali ambayo imefanya wadau wa uongozi wa Serikali za Mitaa, kujiuliza maswali mengi juu ya hatma ya uchaguzi huo mwaka huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Kikundi hicho, Regina Katabi alisema lengo la kutoa tamko hilo ni kutoa changamoto kwa Serikali ya kuona umuhimu wa kila jambo kulichukulia kwa umuhimu wake.
Aliwataka wananchi kushiriki katika mchakato wa Katiba kwa uhuru kuanzia utafutaji wa Katiba mpya hadi Uchaguzi Mkuu 2015.

No comments: