WENYE MADENI UDOM WARUHUSIWA KUFANYA MITIHANI

Serikali imewahakikishia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) walioshindwa kulipa ada  kwamba watafanya mtihani na kama yapo madeni, watayalipa baada ya kumaliza.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa msimamo huo jana kutokana na swali la  Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) aliyesema zipo taarifa, wanafunzi  500 wa chuo hicho wamezuiwa kufanya mitihani yao kwa kushindwa kulipa ada za mitihani.
“Je, Serikali inachukua hatua gani kuwasaidia?” alihoji mbunge huyo katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Pinda alisema Serikali itahakikisha wanafunzi hao, wanaruhusiwa kufanya mitihani yao na kama kuna madeni wanayodaiwa, watayalipa baada ya kumaliza mitihani hiyo.
Alisema yeye na serikali, watafuatilia kwa karibu kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi. “Ni imani yangu na sidhani kama tutaruhusu wanafunzi hao, washindwe kufanya mitihani kwa sababu ya suala la  ada,” alisema.
Alisisitiza, hata kama baadhi yao, watakuwa wamelipa nusu ya ada, au wengine hawajalipa kabisa, watafanya tu mitihani hiyo.
“Haiwezekani mtu asome chuo kikuu miaka mitatu au minne, halafu anafika kwenye mitihani ya mwisho anazuiliwa kufanya mitihani. Tutalitafutia ufumbuzi wa haraka suala hili”, alisema. Aidha alimshukuru mbunge kwa kumpa taarifa ambayo kwa mujibu wake, hakuwa nayo.

No comments: