ALIYEMNG'ATA MSICHANA WAKE WA KAZI APANDISHWA KORTINI

Mwanamke aliyekuwa akituhumiwa kumng’ata msichana wake wa kazi sehemu mbalimbali za mwili, Amina Maige (42), mkazi wa Mwananyamala, Dar es Salaam amefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kudhuru mwili.
Wakili wa Serikali, Mohamed Salum mbele ya Hakimu Yohana Yongolo, alidai Amina alitenda kosa hilo Januari  na Juni mwaka huu, alimng’ata Yusta Kashinde sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Amina alikana mashitaka na Mahakama ilielezwa upelelezi wa kesi umekamilika. Alinyimwa dhamana kutokana na Mahakama kuhofia usalama wake na kesi itatajwa tena Juni 26 mwaka huu.
Mama huyo wakati anaingia mahakamani jana, alizongwa na watu wakiwemo waliokuwa wakimzomea, hali iliyomlazimu kuziba uso kwa mtandio na kusababisha aanguke.
Baadhi ya watu walionekana kutaka kumshambulia kwa kipigo, hali iliyosababisha askari Polisi kuingilia kati ili kuwadhibiti.
Wakati akitoka mahakamani baada ya kesi kuahirishwa, baadhi ya watu waliokuwepo mahakamani hapo walimzomea na wengine wakiimba kuhimiza haki itendeke.

No comments: