MKAPA ADAI VIONGOZI WA SASA AFRIKA SI WAJASIRI

Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema hivi sasa hakuna viongozi wa Afrika wenye ujasiri na uthubutu kama walivyokuwa viongozi waasisi waliopigania uhuru wa nchi za Afrika na kukataa utawala wa kikoloni.
Mkapa alisema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwenye wa mdahalo  wa masuala ya uchumi ulioshirikisha wasomi, viongozi, wanadiplomasia na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mdahalo huo wenye mada: ‘Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Umoja wa Ulaya (EPA); Je, Afrika inanufaika vipi?’ uliongozwa na Profesa Yash Tandon, ambaye ni mwanaharakati kutoka Uganda wa masuala ya siasa.
Rais huyo mstaafu alisema, hakuna viongozi wenye kariba na ujasiri wa viongozi wa Afrika waliokuwepo enzi za kupigania uhuru na kukataa ukoloni kama Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Kenneth Kaunda.
Alisema viongozi wa sasa wanafikiria kisiasa na wanaamini kila jambo linaweza kutafutiwa ufumbuzi wa kisiasa.
“Nani ni kiongozi kama kina Nyerere, Mandela, Kaunda, Gamal Nasser ambao waliongoza ushindi wa kwanza dhidi ya ukoloni. Hatuna viongozi sasa Afrika wanaoweza kuongoza mapambano dhidi ya ukoloni unaofanywa sasa na nchi za Ulaya,” alisema.
Rais Mkapa akichangia katika mdahalo huo alionya nchi za Afrika kutokubali kudanganyika. Alizitaka kutokufanya haraka kusaini  mkataba wa EPA.
“Wenzetu wa Afrika Magharibi walifanya utafiti wao wa kina na kugomea kusaini makubaliano hayo, ndivyo tunavyotakiwa kufanya hivyo Afrika Mashariki, tupaze sauti kukataa kudanganyika. Ninachoamini kanda za Afrika zinaweza kushirikiana vizuri kiuchumi bila kushirikisha nchi za Umoja wa Ulaya,” alisema.
Kwa mujibu wa Mkapa, kwa masharti yaliyotolewa kwenye makubaliano ya EPA ambayo nchi za Afrika zimepewa tarehe ya mwisho kusaini Septemba, mwaka huu, ni dhahiri Afrika iko kwenye ukoloni  kwa kile alichoeleza, nchi hizi hazijapewa muda wa kutosha kufikiria na kuchambua kwa kina kuhusu makubaliano hayo na badala yake zimekuwa zikishinikizwa kusaini.
Alihadharisha kuwa kama nchi za Afrika zitakubali kuweka saini katika mikataba hiyo ya kiuchumi na Umoja wa Ulaya, upo uwezekano wa uchumi wa nchi hizo kudumaa kwa muda mrefu.
Alitoa sababu ya uwezekano wa kudumaa ni kwa sababu ushirikiano huo utaua mwingiliano wa kikanda, biashara huru kwa washirika wa nchi za Afrika.
Pia wajasiriamali wadogo na wa kati wa Afrika hawatakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zitakazoweza kuingia katika ushindani na bidhaa kutoka nchi za Ulaya.
Aidha alisema, viwanda vya ndani vitashindwa kuendelea na ushindani kwenye soko la wazi dhidi ya mataifa yaliyoendelea.
Profesa Tandon kwa upande wake alisema ameshtushwa na hatua ya maofisa wa Afrika walioshiriki katika mazungumzo kukubali kusainiwa kwa EPA. Alisema wamekuwa wakidanganyika na lugha za kitaalamu zinazotumika kuwashawishi kukubali bila kufanya utafiti wa kina.
“Nasema viongozi wa Afrika watafanya kosa kubwa kukubali kusaini makubaliano hayo ambayo matokeo yake yatakandamiza uchumi wa Afrika. Waafrika wanalilia bure tu, wakati wasiposaini mkataba huo hakuna tatizo lolote litakalotokea kwa nchi za Afrika kutosaini mikataba hiyo ya ushirikiano,” alisema.
Profesa Tandon alisema kama Waafrika hawatakuwa makini wanaweza kujikuta wakitawaliwa mara ya pili.

No comments: