KESI YA KIKATIBA YAPANGIWA JOPO LA MAJAJI

Kesi ya kikatiba iliyofunguliwa kutaka Mahakama iruhusu mbunge aliyefukuzwa uanachama katika chama chake atambuliwe kuwa mbunge huru au aruhusiwe kuhama na ubunge wake kwenda chama chochote, imepangiwa jopo la majaji watatu.
Ilifunguliwa na wananchi watatu Jimbo la Kigoma Kusini, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inatarajiwa kusikilizwa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Waliofungua kesi hiyo na vyama vyao kwenye mabano ni Juma Nzengula (CCM), Patrick Rubilo (NCCR-Mageuzi) na Fanuel Bihole wa CUF kwa niaba ya wananchi wengine wa jimbo hilo. Majaji waliopangwa kuisikiliza ni Jaji Lawrence Kaduri, Salvatory Bongole na Zainab Mruke.
Katika madai yao, wananchi hao wanaiomba Mahakama iamuru kusitishwa kwa matumizi ya Ibara ya 71 (1) (f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mbunge aliyefukuzwa uanachama katika chama chake.
Wanataka pia Mahakama iamuru Bunge litunge sheria inayoruhusu mbunge aliyefukuzwa uanachama katika chama chake atambuliwe kuwa mbunge huru au aruhusiwe kuhama na ubunge wake kwenda chama chochote atakachotaka.
Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao kupitia Kampuni ya Uwakili ya Mpoki & Associates, wanadai ibara hiyo inakiuka haki za msingi zinazoelezwa katika Ibara ya 21 ya Katiba inayotoa uhuru wa kushiriki katika shughuli za umma kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Ibara hiyo inakiuka Ibara ya 201 (1) ya Katiba inayotoa uhuru kwa wananchi kushiriki na kutoa maoni kwa uwazi, pia inakiuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu ambao Tanzania imeuridhia na kuusaini.
Kesi hiyo ilifunguliwa siku chache baada Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kuvuliwa uanachama wa NCCR-Mageuzi, hatua ambayo kikatiba ilikuwa inamvua ubunge wake.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kafulila alisema hiyo siyo kesi ya NCCR bali inahusu upungufu wa katiba ya nchi na inaonesha umuhimu wa katiba mpya na kuongeza kuwa  waliifuta baada ya kumalizana nje ya Mahakama na kwa sasa yeye ni mwanachama hai pia ni Katibu Mwenezi Taifa wa chama hicho.
Alisema anaunga mkono kesi hiyo kwa kuwa inaonesha udhaifu wa Katiba ambao vyama vya upinzani wamezungumza kwa muda mrefu.

No comments: