BUKOBA WAPEWA MAFUNZO KUJIKINGA NA DENGUE

Wakazi wa Mkoa wa Kagera wamehadharishwa juu ya ugonjwa wa dengue kwa kutakiwa kuweka mazingira katika usafi.
Wametakiwa kusafisha mazingira ya nyumba na mifereji inayozunguka nyumba zao, kufyeka nyasi na vichaka  karibu na makazi.
Aidha wameelekezwa maua yanayopandwa kwenye makopo, wahakikishe maji hayatuami kuepuka kuruhusu mbu waenezao ugonjwa huo kuzaliana.
Ofisa Afya wa Mkoa wa Kagera, Herman  Kabirigi, alitoa maelekezo hayo juzi mjini hapa kwenye mkutano wa wadau kujadili namna ya kujikinga na ugonjwa huo. 
"Endapo wananchi watazingatia njia zinazotolewa na wataalamu, hatutakumbwa na ugonjwa wa dengue. La muhimu ni kuweka mazingira katika hali ya usafi,” alisema.
 Alisema endapo mtu atahisi  kupatwa na dalili za ugonjwa huo, awahi kwenye kituo cha afya. Miongoni mwa dalili ni homa kali, kuumwa kichwa, kichefuchefu au kutapika, maumivu ya misuli, uchovu, pamoja na  harahara au vipele vidogo.
Kwa mujibu wake,  baada ya Mkoa wa Kagera kupata taarifa juu ya kuwepo mlipuko wa ugonjwa huo, mamlaka za serikali za mitaa zilipewa taarifa zichukue hadhari ikiwa ni pamoja na kuelimisha umma juu ya ugonjwa huo, jinsi unavyoenea na jinsi ya kujikinga.

No comments: