TIB, EPZA WASAINI MKATABA WA MKOPO

Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) imesaini makubaliano na Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) kwa ajili ya kupata mikopo ya kujenga miundombinu itakayovutia wawekezaji kuanzisha viwanda katika maeneo yake maalumu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Adelhelm Meru aliwaambia waandishi wa habari baada ya kusaini mkataba huo, kuwa makubaliano hayo yanalenga kuendeleza maeneo ya mamlaka hiyo yaliyosambaa pote nchini.
“Makubaliano haya ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu,” Dk Meru aliwaambia waandishi wa habari jana.
Alisema kupitia makubaliano hayo maeneo maalumu ya uwekezaji kama Bagamoyo, Mtwara, Kigoma, Tanga na mengine yote yaliyo katika mikoa 20 yatapata miundombinu itakayovutia wawekezaji wa ndani na nje.
Alisema makubaliano hayo yanalenga kutimiza ndoto ya muda mrefu ya kujenga miundombinu katika maeneo hayo.
“Hii ni dalili nzuri kwa vile kwa sasa badala ya kuomba fedha Mfuko wa Serikali au kutoka nje ya nchi, sasa nchi yetu ina benki yenye uwezo wa kugharimia miradi mbalimbali,” alisema Dk Meru.
Alifafanua kwamba wawekezaji wanapenda kuwekeza katika maeneo ambayo tayari yana miundombinu na hivyo kwa kuchukua hatua hiyo wengi watavutiwa na maeneo hayo na kuiletea nchi faida.
Aliongeza kusema kuwa viwanda vikianzishwa katika maeneo hayo Watanzania wengi watapata ajira, mapato yataongezeka na uchumi wa nchi utaimarika zaidi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Peter Noni alisema benki yake tayari imejenga uwezo wa kifedha wa kutosha kwa ajili ya kusaidia miradi ya ujenzi ya miundombinu itakayovutia wawekezaji kujenga viwanda.
“Tunatambua maeneo maalumu ya mamlaka hii ni ya kitaifa na yanahitaji kuendelezwa kuvutia uwekezaji, ni wajibu wetu kutekeleza jambo hili,” alisema.
Alisema Wizara ya Nishati na Madini inatarajia kuongeza uzalishaji wa umeme kufikia megawati 3,000 baada ya mwaka mmoja, na hivyo ni vyema kuwa na miundombinu inayovutia uwekezaji kuja kujenga viwanda nchini.
“Kwa muda mrefu tumekuwa hatuna viwanda vingi kutokana na umeme kutokuwa na uhakika, sasa uhakika huu upo,” alisema, na kuongeza kuwa mkataba huo ni moja ya matayarisho hayo.
Alisema benki hiyo imeamua kushirikiana na mamlaka hiyo kwa vile tayari ina maeneo maalumu na ni vyema yaandaliwe mapema kwa kujengwa miundombinu inayotakiwa na wawekezaji.

No comments: