ULINZI MKALI KWA WATUHUMIWA WA BOMU LA ARUSHA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, jana ilipewa ulinzi mkali wa Polisi  wakati watuhumiwa  tisa wa mlipuko wa bomu, uliotokea baa ya Arusha Night Park, walipofikishwa mahakamani hapo.
Wakati askari wenye mbwa wakiranda kwenye maeneo ya Mahakama, kulikuwa na upekuzi kabla ya kuingia ndani ya chumba cha Mahakama ambako watu hao walisomewa mashitaka 16 ya kujaribu kuua na kuua.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi,  Mustapher Siyani, waliosomewa mashitaka ni Abdallah  Rabia (34), mkazi wa Karatu, Abdulkarim  Hasia (32) mkazi wa Ngusero, (yupo wadini), Ally  Kidanya  (32) na Rajabu Hemedi (28) ambao ni wakazi wa Magugu, Babati.
Wengine ni, Abdallah Wambura (40) mkazi wa Kwa Murombo (yupo wadini),  Ally Jumanne (25), Hassan Said (23) mkazi wa Tengeru, Shabani Wawa (22) mkazi wa Magugu   na Yassin Sanga.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Wakili Hellen Rwijage, alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 25 mwaka huu ili  kuwaunganisha na washitakiwa wanane wanaodaiwa kushawishi vijana kuingia katika kikundi cha kigaidi cha al-Shabaab.
Washitakiwa hao wanadaiwa Aprili, 13 mwaka huu saa 1:30 usiku, kwenye baa ya Night Park, walilipua bomu na kusababisha majeruhi na kifo cha Sudi  Ramadhani.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na Mamlaka ya kusikiliza kesi husika.

No comments: